Huduma tatu zilizoboreshwa kwenye kitambulisho kipya cha NIDA

November 18, 2026 5:39 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • NIDA yasema vitambulisho vya zamani vinaendelea kutumika, zaidi ya milioni 1.8 bado havijachukuliwa na wamiliki wake. 

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, amesema kitambulisho kipya cha Taifa cha mwaka 2026 kimefanyiwa maboresho katika maeneo matatu ambayo ni usalama, uimara na uwezo wa matumizi, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Kaji aliyekuwa akizungumza leo Novemba 18, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitambulisho hicho Kibaha, mkoani Pwani, ameeleza kuwa maboresho hayo yanalenga kukifanya kitambulisho hicho kuwa na uwezo mpana zaidi wa kumtambulisha mwananchi na kumuunganisha na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Kadi mpya ina vipengele vya kisasa vya kiusalama vikiwemo alama zinazobadilika kulingana na mwanga wa joto, alama zinazotambulika kwa mguso na vipengele vingine…,” amesema Kaji.

Aidha, amebainisha kuwa teknolojia hizo zitasaidia kupunguza uwezekano wa kughushi vitambulisho na kuimarisha uaminifu wa taarifa za utambulisho wa mwananchi.

Katika eneo la pili la uimara, Kaji amesema NIDA imehamia katika teknolojia ya ‘laser engraving’, inayowezesha taarifa na picha za mwananchi kuchongwa ndani ya tabaka la kadi badala ya kuchapishwa kwa wino juu ya uso wake.

Amesema teknolojia hiyo itasaidia kuzuia taarifa na picha kufutika au kuharibika kirahisi kama ilivyokuwa kwa baadhi ya vitambulisho vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya awali.

Akielezea eneo la tatu la uwezo wa matumizi, amesema kitambulisho kipya kimeongezewa teknolojia ya ‘Machine Readable Zone (MRZ)’ na msimbo wa ‘QR Code’, vitakavyowezesha taarifa za mwananchi kusomwa na kuthibitishwa kupitia mifumo husika.

Hata hivyo, kitambulisho hicho kimeongezewa nafasi za programu za kidijitali kutoka nne zilizokuwepo awali hadi nane, hivyo kuongeza mara mbili uwezo wa kuunganisha huduma mbalimbali kwenye kadi hiyo.

Katika maelezo yake, huduma zinazolengwa kuunganishwa ni pamoja na bima ya afya, leseni ya udereva, uthibitishaji wa utambulisho na huduma nyingine za kidijitali, ikiwemo matumizi katika baadhi ya mifumo ya usafiri kama SGR na mabasi ya mwendokasi.

Kwa mujibu wa Kaji, mfumo huo pia unalenga kukusanya taarifa muhimu zinazohusu cheti cha kuzaliwa, ndoa, talaka na vifo, hatua inayotarajiwa kuboresha utunzaji wa taarifa za utambulisho wa wananchi. 

Maboresho hayo yalifanyika kwa hatua, ambapo mwaka 2016 NIDA iliongeza vipengele vya utambuzi na usalama katika vitambulisho, kabla ya mwaka 2019 kufanya maboresho mengine kwa kuanza kutumia teknolojia ya ‘drop on demand’, iliyowezesha uchapishaji wa taarifa na picha za mwananchi kwenye kadi kwa kutumia wino. 

Kitambulisho kipya hakibatilishi uhalali wa cha zamani 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amefafanua kuwa uzinduzi wa kitambulisho kipya cha Taifa hauondoi uhalali wa vitambulisho vya awali, hivyo wananchi wenye vitambulisho vya zamani ambavyo havina dosari hawana sababu ya kukimbilia kuvibadilisha.

Akibainisha hilo Katambi amesema, vitambulisho vipya vitatolewa kwa wananchi wanaojiandikisha kuanzia sasa, huku wenye vitambulisho vya awali wakiendelea kuvitumia katika kupata huduma mbalimbali hadi pale vitakapoharibika na kufuata utaratibu wa kubadilishiwa.

“Aliye na cha zamani na aliye na hiki kipya vyote ni vitambulisho na vinatambulika, isipokuwa huyu mwenye kipya atakuwa na sifa ya ziada ya sifa ambazo zimeongezwa kwenye kitambulisho hicho,” amesema Katambi.

Katika hatua nyingine, amewataka wananchi ambao tayari wana namba za NIDA lakini hawajachukua vitambulisho vyao kufika katika ofisi za mamlaka hiyo kuvichukua, akieleza kuwa zaidi ya vitambulisho milioni 1.8 bado havijachukuliwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
18 Nov, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
18 Nov, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
18 Nov, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
RC Chalamila: Nyumba za ibada zijengwe kwa kuzingatia mipango miji.

RC Chalamila: Nyumba za ibada zijengwe kwa kuzingatia mipango miji.

Nukta TV

JKT: Nafasi haziuzwi, hakuna upendeleo wala kurudia mafunzo

JKT: Nafasi haziuzwi, hakuna upendeleo wala kurudia mafunzo

Nukta TV

Noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa haraka, nini kifanyike? wananchi wafunguka

Noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa haraka, nini kifanyike? wananchi wafunguka

Nukta TV