Sababu 5 zinazowafanya vijana kujitoa uhai
- Ni pamoja na changamoto za kimazingira na ukuaji wa ubongo.
Dar es Salaam. Hebu subiri kidogo hivi, umewahi kujiuliza ni nini kinachoweza kumfanya kijana afikie hatua ya kuona kwamba maisha yake hayana tena thamani duniani?
Nyuma ya tabasamu tunaloliona kila siku, kuna vijana wanaopitia changamoto nzito za kihisia, kisaikolojia na kijamii ambazo mara nyingi hazionekani kwa macho.
Changamoto hizo kwa namna moja au nyingine zinaweza kumfanya mtu afikirie kujitoa uhai akiamini kuwa baada ya yeye kuondoka duniani kila kitu kitakuwa sawa.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kujitoa uhai ni tatizo kubwa la afya ya umma linalohitaji hatua za pamoja katika ngazi ya jamii na taifa, likikadiriia vifo vya takribani watu 746,000 kila mwaka vinavyotokana na changamoto hiyo.
Mbali na vifo hivyo, WHO, imebainisha kuwa mwaka 2023, kujitoa uhai kulikuwa sababu ya pili ya vifo miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 29 duniani kote.
Lakini sababu kuu ya vijana kujitoa uhai ni nini?
Daktari bingwa bobezi wa afya ya akili kwa watoto na vijana kutoka Taasisi ya Afya ya Akili Tanzania(TMHI) Godwin Mwisomba amesema kujitoa uhai kwa vijana hususani wenye miaka 15 hadi 29 hutokana na mlundikano wa changamoto za kisaikolojia, kijamii, na kibaiolojia zinazozidi uwezo wa kijana kuhimili.
Kwa mujibu wa Dk Mwisomba, moja ya sababu ya vijana kujiua ni ukuaji wa ubongo ambao bado haujakamilika hususani sehemu inayohusika na kufanya maamuzi sahihi, kutatua matatizo na kudhibiti misukumo ya ghafla (prefrontal cortex) ambayo huendelea kukomaa hadi katika utu uzima wa awali.
“Kwa kuwa sehemu ya ubongo inayodhibiti maamuzi na msukumo wa ghafla (prefrontal cortex) hukomaa karibu na miaka 25 huku sehemu ya hisia ikiwa na nguvu kupita kiasi, vijana huhisi maumivu na kukataliwa kwa uzito mkubwa, hushindwa kuona kuwa tatizo ni la muda, na hufanya maamuzi ya ghafla,”
Hali hii inaweza kuwafanya vijana kupata maumivu ya kihisia kwa kiwango kikubwa, kuathirika sana wanapokataliwa au kukatishwa tamaa, kushindwa kuona suluhisho mbadala wanapokabiliwa na changamoto, kufanya maamuzi ya ghafla bila kutafakari matokeo yake.
Katika mazingira ya msongo mkubwa wa mawazo au kukata tamaa, hali hii inaweza kuongeza hatari ya kupata mawazo ya kujitoa uhai.

Changamoto za kijamii na mazingira
Mtaalamu wa Saikolojia Tiba na Mahusiano, Leyla Abubakari kutoka mkoani Tanga ameieleza Nukta Habari kuwa kwa baadhi ya vijana, mazingira ya kijamii wanayoishi yanaweza pia kuchochea maamuzi ya kujiua.
Leyla amezitaja changamot hizo kuwa ni unyanyasaji, ukatili wa kijinsia, uonevu, ubaguzi na migogoro ya kifamilia inayoweza kuwaacha na majeraha ya kihisia.
Hali huwa mbaya zaidi pale kijana anapokosa mtu wa kumweleza kutokana na hofu ya kuhukumiwa au kubezwa na watu wanaowazunguka.
“Baadhi ya vijana wanapokumbana na matatizo hukosa watu wanaoweza kuwasikiliza, kuwashauri au kuwapa faraja. Wengine huogopa kuhukumiwa wanapojaribu kueleza hisia zao, hivyo kuamua kubeba maumivu yao kimyakimya,” anaeleza Leyla.
Mtaalamu huyo ameongeza kuwa sababu nyingine ya vijana kujiua ni kujilinganisha na marafiki katika masuala ya elimu, kazi, kipato na matumizi ya mitandao ya kijamii yaliyokithiri yanayoweza kuathiri hali ya kihisia ya vijana.

Sonona na matumizi ya vilevi
WHO, imebainisha uhusiano kati ya baadhi ya hali za afya ya akili ikiwemo sonona pamoja na matumizi ya vilevi kiwemo pmbe kuwa miongoni mwa sababu za kujiua.
Hali hiyo inaelezewa na Dk Mwisomba kuwa chanzo cha kuharibu uwezo wa kufikiri na kuongeza kukata tamaa ambavyo vyote huweza kupelekea kijana kujiua.
Mtaalamu huyo amezitaja hali nyingine za afya ya akili kama majeraha ya ubongo na ugonjwa wa spektra ya usonji kuhitaji uangalizi maalumu wa kiafya ili zisiwe sababu ya kijana kupoteza maisha.
Vichocheo vya ghafla
Matukio ya ghafla kama kuvunjika kwa mahusiano ya kimapenzi, kufeli mitihani, kupoteza mtu wa karibu, migogoro ya kifamilia, au kudhalilishwa mbele za watu yanayomkuta kijana yanaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia kuathirika kwa afya yake ya akili na kumfanya afikirie hatua kujitoa uhai.
Matukio hayo yanapokuwa mazito kihisia, yanaweza kumfanya ashindwe kuona namna ya kukabiliana na changamoto anazopitia.
Dk Msobwa anasema athari za matukio hayo zinaweza kuwa kubwa zaidi pale kijana anapokuwa na msongo wa mawazo na mazingira yanayorahisisha kujidhuru.
“Majanga ya ghafla kama vile kuvunjika kwa mahusiano au aibu hadharani huweza kuleta madhara makubwa kunapokuwa na upatikanaji rahisi wa vitu hatari (sumu/visu/dawa za kawaida) na unyanyapaa unaozuia kupata msaada.”

Kushindwa kufikia malengo
Leyla anaongeza kuwa, kwa baadhi ya vijana kushindwa kutimiza malengo walijipangia kunaweza kuongeza hatari ya vijana kufikiria kujitoa uhai.
Anaeleza kuwa baadhi ya vijana wanapoweka matarajio makubwa katika masomo, biashara au ajira lakini wakashindwa kuyafikia, huweza kujiona hawana mafanikio na kupoteza matumaini ya maisha.
Lakini ikumbukwe kuwa kujitoa uhai pia kuna weza kuambukizwa.
Hali hii hutokea pale ambapo taarifa au tukio la mtu kujitoa uhai linapoweza kuongeza hatari ya watu wengine katika jamii, shule au sehemu za kazi kuathirika kwa namna inayoweza kuwafanya nao wafikirie kujitoa uhai.
Vijana wanaweza kuathiriwa moja kwa moja wanapofiwa na rafiki au ndugu kwakujitoa uhai au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia taarifa zinazosambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.