ASAS Energies kuinunua Oryx Gas Tanzania
- Iwapo muamala huo utakamilika, ASAS itakuwa imejihakikishia umiliki wote wa kampuni hiyo kubwa zaidi kwenye soko la gesi nchini.
Dar es Salaam. Kampuni ya ASAS Energies Limited imetangaza nia ya kununua asilimia 100 ya hisa za Oryx Gas Tanzania Limited, hatua itakayoongeza umiliki wake kwenye biashara ya gesi ya kupikia na kupanua wigo wake katika sekta ya nishati nchini.
Mpango huo umebainishwa na Tume ya Ushindani (FCC) kupitia tangazo la Novemba 10, 2026, lililoeleza kuwa imepokea na kuanza kuchambua taarifa ya muunganiko wa kampuni hizo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, ASAS Energies inakusudia kununua hisa zote za Oryx Gas kutoka kwa kampuni ya Oryx Energies SA kupitia Mkataba wa Ununuzi wa Hisa na Dhamana ulioingiwa kati ya wahusika hao.
Hata hivyo, hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku 20 tangu Oktoba 21, 2026, Oryx Energies ilipotangaza kuingia makubaliano ya kuuza biashara yake ya gesi Tanzania kwa ASAS, ikiwa ni sehemu ya mapitio ya kimkakati ya uwekezaji wake katika shughuli za biashara ya bidhaa za petroli kwa watumiaji wa mwisho barani Afrika.
Iwapo muamala huo utakamilika, ASAS itakuwa imejihakikishia umiliki wote wa kampuni hiyo kubwa zaidi kwenye soko la gesi nchini hatua itayoiongezea umiliki wa biashara ya kuhifadhi, kujaza na kusambaza gesi ya kupikia (LPG) kwa matumizi ya majumbani na kwenye vyombo vya moto.
Katika soko la gesi nchini, takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) za Robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26 zinaonyesha kampuni ya Oryx ilikuwa na asilimia 36.78 ya soko la LPG, ikifuatiwa na Taifa Gas yenye asilimia 22.23 na Puma Gas asilimia 11.45.
Hata hivyo, muamala huo bado haujakamilika, kwani unasubiri tathmini na vibali vinavyohitajika kutoka mamlaka za udhibiti.
FCC imewaalika wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine kuwasilisha maoni kuhusu uwezekano wa ununuzi huo kupunguza ushindani au kuathiri walaji, wasambazaji, washindani na wafanyakazi.
Wakati ASAS wanapanga kuichukua Oryx Gas, AMSONS Industries nayo inakamilisha taratibu za kununua Oryx Energies iliyokuwa kampuni mama ya Oryx Gas ambayo nayo inasubiri baraka za FCC kukamilisha dili hilo.