Lindi kinara ajira nyingi za Serikali kuliko binafsi
- Licha ya kuwa na ajira nyingi za sekta ya umma, mikoa 11 inayoongoza kwa ajira hizo ina jumla ya ajira sawa na nusu tu ya ajira za sekta zote zilizopo Dar es Salaam pekee.
Dar es Salaam. Licha ya sekta binafsi kuwa na mchango mkubwa katika kuajiri ikichangia zaidi ya asilimia 70 ya ajira zote nchini, bado kuna mikoa 11 ambayo inaongoza kwa kuwa na wafanyakazi wengi zaidi walioajiriwa katika sekta ya umma kuliko binafsi.
Ripoti ya Kitabu cha Uchumi ya mwaka 2023/24 imeutaja mkoa wa Lindi kuwa kinara kwa idadi ya ajira katika sekta ya umma nchini, ukirekodi ajira 42,326 kwa mwaka huo wa fedha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayotolewa na Wizara ya Fedha, idadi hiyo ya ajira ni zaidi ya mara tatu ya ajira 13,769 za sekta binafsi zilizorekodiwa katika kipindi sawa na hicho ndani ya mkoa huo.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa hii si mara ya kwanza kwa mkoa wa Lindi kurekodi ajira nyingi zaidi kwenye sekta ya umma kuliko sekta binafsi.
Rekodi zilizopo kwenye kitabu cha uchumi, zinaonyesha kuwa Lindi imeendelea kuchangia wastani wa asilimia 1.1 ya ajira zote za sekta ya umma nchini kwa miaka sita mfululizo tangu mwaka wa fedha 2019/20, huku mchango wake katika ajira za sekta binafsi ukibaki katika wastani wa asilimia 0.3 katika kipindi hicho.
Mazingira ya uwekezaji kikwazo
Kwa mtazamo wa kiuchumi, mchango wa asilimia 0.3 wa Lindi katika ajira za sekta binafsi nchini bado uko chini ni kulinganisha na ukubwa wa sekta hiyo inayochangia zaidi ya asilimia 70 ya ajira zote nchini.
Wizara ya Fedha inasema kuwa hali hiyo katika mkoa wa Lindi ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya usafirishaji na umeme wa uhakika inachangiwa na muundo wa uchumi na mazingira ya kijiografia ya mkoa huo.
Uchumi wa mkoa Lindi unategemea zaidi kilimo cha kijaji, uvuvi, na ujasiriamali mdogo usio rasmi, jambo linalopelekea uhaba wa uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda vikubwa na kampuni za kibiashara zinazoweza kutoa ajira za mkataba kwa kiwango kikubwa.
Bado ajira hazitoshi
Katika orodha ya mikoa ambayo inaongoza kwa ajira nyingi kwenye sekta ya umma, Lindi imefuatiwa na mkoa wa Katavi uliorekodi ajira 15,701 za umma.
Mikoa mingine ilinayofuatia ni pamoja na Shinyanga iliyorekodi ajira 81,505, Kagera ajira 50,929, Njombe ajira 32,026, Mara ajira 47,845, Manyara ajira 32,716 , Simiyu ajira 22,891, Geita ajira 33,866, Songwe na Singida ajira 19,991 na 36,287 mtawalia.
Licha ya mikoa hii kuwa na idadi kubwa ya ajira katika sekta ya umma bado jumla ya ajira zilizopo ni chache kulinganisha na idadi ya watu pamoja na uhitaji uliopo.
Jumla ya idadi ya ajira zilizopo katika mikoa yote 11 inayoongoza kwa ajira za umma ni nusu tu ya jumla ya ajira zote 1,371,640 zilizopo katika mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Imeandikwa na Method Allen, nyongeza na Kelvin Makwinya.