Tanzania yagundua kiwango kingine cha gesi asilia Mtwara
- Yagundua futi za ujazo bilioni 223 ikiwa ni ni ugunduzi mpya kwa zaidi ya miaka 10 baada ya ugunduzi wa mwisho uliofanyika mwaka 2015.
- Ugunduzi huuo umefanyika katika kisima cha utafutaji cha Kasa-X1 ST2 kinachoendeshwa na TPDC na Maurel and Prom.
Dar es Salaam. Tanzania imegundua gesi asilia inayokadiriwa kuwa futi za ujazo bilioni 223 katika kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara ikiwa ni ugunduzi mpya baada ya miaka 10, hatua itakayoongeza upatikanaji wa nishati hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi.
Waziri wa Nishati Dk Juma Homera amesema kiwango hicho kipya cha gesi asilia kiligunduliwa baada ya kuchoronga kisima kiitwacho Kasa-1X ST2 kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya Maurel & Prom (M&P).
Ugunduzi huo mpya uliobainika Kusini mwa Tanzania utaongeza kiwango cha hifadhi ya gesi asilia (natural gas reserve) kufikia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57.76. Kablsa ya ugunduzi mpya, Tanzania ilikuwa na hifadhi ya gesi asilia futi za ujazo wa trilioni 57.54 kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Dk Homera amesema nguvu ya maamuzi na ushawishi wa TPDC katika kitalu hicho cha Mnazi Bay imekuwa sababu ya uchorongaji wa visima vitatu kwa kushirikiana na mbia wake huyo M&P.
“Visima viwili (MB-5 na MS-2) vimeongeza uzalishaji kwa takribani zaidi ya futi za ujazo milioni 65 kwa siku, na kisima cha Kasa-1X ST2 pekee kinatarajiwa kuzalisha futi za ujazo milioni 30 kwa siku kwa miaka isiyopungua 10,” amesema Dk Homera katika hafla ya kutangaza ugunduzi huo mkoani Mtwara.
“Nawapongeza tena TPDC na M&P kwa uthubutu na fikra za kibiashara zilizopelekea uamuzi huu wa uwekezaji.

Ongezeko la uzalishaji wa gesi asilia, amesema, linatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia mgawo wa Gesi ya Faida (Profit Gas) kwa mujibu wa Mkataba wa Ugawanaji wa Mapato ya Petroli (PSA), mapato ya TPDC kama mbia, na kodi mbalimbali.
Kiongozi huyo wa wizara amesema aidha, shughuli za kiuchumi zinazohusiana na mradi zitachangia kuongeza mapato ya halmashauri za mkoa wa Mtwara.
Ugunduzi huo wa gesi na ongezeko la uzalishaji, Dk Homera amesema vinaimarisha imani ya wawekezaji na kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.

“Kufuatia ugunduzi huu, TPDC imeingia katika majadiliano na wawekezaji wanne (4) wanaopanga kuendeleza miradi midogo ya gesi asilia kimiminika (LNG), ambapo watatu (3) wanatarajiwa kutekeleza miradi yao Mtwara. Miradi hiyo itaongeza ajira na kuchochea matumizi ya gesi asilia kwenye magari kama mbadala wa petroli na dizeli,” amesema.
Tanzania imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya utafutaji wa gesi na mafuta ya petroli nchini kwa zaidi ya miaka 50. Ugunduzi wa mwanzo wa gesi asilia nchini ulifanywa mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi na kufuatiwa na ugunduzi mwingine Mnazi Bay miaka nane baadaye.

Sehemu kubwa ya gesi asilia nchini hutumika katika uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwanda, majumbani na katika majengo ya biashara na katika vyombo vya moto ikiwa ni sehemu ya kupunguza matumizi makubwa ya nishati isiyo salama kwa mazingira.
Hadi Machi 2026, gesi asilia ilikuwa inachangia uzalishaji wa umeme kwa megawati 721 ikiwa ni takriban theluthi ya uzalishaji wote wa umeme, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, kiwango ambacho kimeshuka kutokana na kuwashwa kwa kituo cha kuzalishia umeme cha Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).