Kadhaa wahofiwa kupoteza maisha, jengo la zaidi ya ghorofa 10 likiporomoka Kenya
- Mpaka sasa bado haijajulikana ni vifo vingapi vimesababishwa na nini hasa chanzo cha ajali hiyo.
Dar es Salaam. Watu kadhaa wahofiwa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa kufuatia kuporomoka kwa jengo la zaidi ya ghorofa 10 lililokuwa likiendelea na ujenzi katika Mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi nchini Kenya.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya ikiwemo KBC na K24 jengo hilo limeanguka leo Oktoba 23, 2026 majira ya alasiri huku chanzo cha ajali hiyo kikiwa bado hakijajulikana.
Mpaka sasa, Jeshi la Polisi nchini humo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uokozi vimefika eneo la tukio na shughuli za uokoaji bado zinaendela. Hata hivyo, mpaka sasa bado haijafahamika ni watu wangapi wamepoteza maisha.
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Nairobi, Issa Mohamed waliofika eneo la tukio wametoa amri ya kufungwa kwa shughuli zote katika maeneo yanayozunguka eneo hilo wakitoa tahadhari juu ya uwezekano wa jengo lingine kuporomoka.