DCI, CDF, IGP wakataa kumtetea Lissu kesi ya uhaini
Dar es Salaam. Mashahidi watatu wa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema) Tundu Lissu, wamekataa kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo inayoendelea katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Mashahidi hao Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura walitakiwa kutoa ushahidi wao kumtetea kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani aliyepo mahabusu kwa zaidi ya siku 500.
Lissu, anayeshtakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, ameiambia Mahakama Kuu leo Septemba 18, 2026 kuwa alifanya mazungumzo na DCI Kingai ambaye alimweleza kuwa yeye hayupo tayari kumtetea.
“Kwa maneno yake amesema yeye (DCI Kingai) yuko na wale wanaoomba na kushangilia nikipatikana na hatia. Kwa hiyo amesema hayuko tayari kuja kutoa ushahidi kwa niaba yangu,” amesema Lissu.
Lissu alitakiwa kuwasimamisha mashahidi 11 kwa ajili ya utetezi katika kesi hiyo inayomkabili akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, vigogo wanne wa Chadema na wakuu wanne wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Hata hivyo, mawakili wa Jamhuri waliwasilisha pingamizi la kuitwa Rais Samia na viongozi wengine wa Serikali. Agosti 21 mwaka huu mahakama iliamuru mashahidi wanne wa Chadema kuanza kutoa utetezi wao huku ikishughulikia suala hilo.
Siku chache baadae mahakama iliridhia wakuu watatu wa vyombo vya usalama pekee kutoa utetezi wao katika kesi ya Lissu ikitupilia mbali ombi la kuwasimamisha viongozi wengine wa juu wa Serikali pamoja na wale waliopita.
Mpaka sasa waliofanikiwa kutoa ushahidi ni watu wanne tu kati ya 11 ambao ni Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara Amani Golugwa, Makamu Mwenyekiti John Heche na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia.
Lissu ameimbia mahakama leo kuwa awali alifanya mazungumzo na DCI aliyemjulisha kuwa CDF na IGP nao hawataweza pia kumtetea.
“Ameniambia pia (DCI Kingai) kuhusu mashahidi wengine wawili ambao Mahakama iliamua wapelekewe wito, kwa maana ya Mkuu wa Majeshi na IGP…Kuhusiana na hao amesema hata watakapo rejea nchini na kupata wito wa Mahakama msimamo wao utakuwa huo huo,” amesema Lissu.
Baada ya mashahidi hao kukataa kumtetea, Lissu amefunga ushahidi akiiomba kufanya hitimisho la hoja za pande zote mbili Septemba 23, 2026, ombi lililokubaliwa na mahakama.