Wanahabari watwishwa zigo kuhamasisha matumizi ya nishati safi Tanzania
- Waishauri Serikali na wadau wa Nishati kutengeneza miundombinu itakayowezesha nishati hiyo kuuzwa kwa bei ya chini kuanzia Sh2,000 ili kuwezesha wananchi wenye hali ya chini kumudu.
Morogoro. Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amefungua rasmi warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na maafisa Mlmawasiliano wa Serikali kuhusu uandishi na uhamasishaji wa masuala ya Nishati Safi ya Kupikia.
Makamba aliyekuwa akizindua warsha hiyo Leo Julai 16, 2026 mkoani Morogoro amesema kuwa wanahabari wanajukumu kubwa la kusambaza taarifa sahihi kuhusu nishati hiyo ili kuongeza watumiaji wake.
“Taarifa zisizosahihi zinaweza kurudisha nyuma jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi…Ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yatawasaidia wanahabari kuandaa habari sahihi,”amesema Makamba.
Warsha hiyo kwa wanahabari inafanyikia ikiwa ni miaka miwili tangu Serikali izindue Mikakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) wenye lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi hadi asilimia 80 kutoka asilimia tisa iliyokuwepo wakati huo.
Ndani ya muda huo, matumizi ya nishati safi yamepaa na kufikia asilimia 28.6 ikisalia miaka nane katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake Mhandisi Anitha Ringia kutoka Wizara ya Nishati amesema kinachokwamisha kufikia lengo la mkakati huo kwa haraka ni uelewa finyu kwa baadhi ya Watanzania pamoja na ukosefu wa fedha.
“Kinachokwamisha hapa ni fedha tu maana kama tungekuwa na fungu la kutosha tungeweza kununua mitungi ya gesi na kuisambaza bure nchi nzima,” amesema Mhandisi Anitha.
Nguvu kazi ihamishiwe vijijini
Warsha hiyo kwa wanahabari inafanyikia kwa siku mbili mkoani Morogoro huku Naibu Waziri Makamba akidokeza kuwa wanajipanga kuandaa tuzo maalum kwa waandishi wa habari wa masuala ya nishati ili kuhamasisha uzalishaji wa maudhui mengi zaidi ya nishati.
Kwa upande wao washiriki wa warsha hiyo wameshauri uhamasishaji mkubwa wa Matumizi ya Nishati hiyo uhamishiwe kwa wakazi wa vijijini ambao wana uelewa mdogo.

“Bado Kuna tatizo kubwa vijijini Kila nyumba utakayoenda huwezi kukosa jiko la kuni…shida siyo uchumi wala Nini ni Imani potofu,'”amesema Afisa Habari Halmashauri ya Shinyanga Richard Bagolele
Pamoja na maoni hayo waandishi wengine wameshauri Serikali na wadau wa Nishati kutengeneza miundombinu itakayowezesha nishati hiyo kuuzwa kwa bei ya chini kuanzia Sh2,000 ili kuwezesha wananchi wenye Hali ya chini kumudu.