130 wakamatwa kwa kuhamasisha uhalifu Tanzania
- Ni baada ya Jeshi la Polisi kufanya ufuatiliaji wa karibu katika mitandao ya kijamii na majukwaa mengine.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema linawashikilia watuhumiwa 130 kwa makosa mbalimbali ya kihalifu ikiwemo kusambaza taarifa za uchochezi.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP David Misime iliyotolewa leo Julai 9, 2026 inabainisha kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya ufuatiliaji wa karibu uliofanyika kupitia mitandao ya kijamii na majukwa mengine kama vile vikao vya ndani.
“Vitendo hivyo vya kihalifu vilikuwa ni pamoja kupanga, kutamka, kuandaa na kusambaza taarifa za uchochezi, kuhamasisha watu kushiriki katika vitendo vya kihalifu vikiwepo kuua baadhi ya viongozi na wananchi, kuchoma shule moto…
…Kulipua transfoma za umeme ili nchi iwe gizani, kuharibu na kupora mali za umma na za watu binafsi sambamba na kuua askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupora silaha,” amesema Msime.
Watuhumiwa hao wanakamatwa ikiwa ni siku mbili baada ya vuguvugu la kuhofiwa kutokea kwa maandamano katika maeneo mbalimbali nchini Julai 7 mwaka huu yakilenga kuishinikiza Serikali kufanya maboresho ya kidemokrasia.
Miongoni mwa maboresho hayo kwa mujibu wa wanaharakati waliokuwa wakihamasisha maandamano hayo mtanmdaoni ni katiba mpya, kumaliza utekaji na kumwachia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu.
Badala ya kufanyika maandamano Wakazi wa jiji la Dar es Salaam walishuhudia ulinzi mkali katika sehemu kubwa ya makazi yao wakati Watanzania wakiendelea kuadhimisha Sikukuu ya Sabasaba.
Huenda kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alilolitoa Juni 26, 2026 bungeni Dodoma akiliagiza Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua watakaohusika kuhamasisha maandamano pamoja na kuimriisha ulinzi na usalama mitandaoni na maeneo mengine.
“Kuanzia kesho (Juni 27, 2026) namuagiza IGP Wambura tuanze kuwaita na kuwahoji, wale ambao vielelezo vyao vipo dhahiri tutawafikisha mahakamani, hatutamfumbia macho mtu wa aina yeyote yule,” alisisitiza Katambi.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa watu wote kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa kuepuka kushiriki katika kuandaa na kusambaza taarifa zenye kuhamasisha vitendo vya kihalifu au kusambaza taarifa unazotumiwa na ambazo huna uhakika nazo wala kujua chanzo chake.