Ulinzi waimarishwa Dar, maduka yachelewa kufunguliwa
- Sehemu kubwa ya barabara jijini Dar es Salaam zina msongamano mdogo huku ulinzi ukiimarishwa kwenye makutano ya barabara kuu.
Dar es Salaam. Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wameshuhudia ulinzi mkali katika sehemu kubwa ya makazi yao wakati Watanzania wakiendelea kuadhimisha Sikukuu ya Sabasaba licha ya uwepo wa mpango wa maandamano.
Baadhi ya watu mitandaoni wamekuwa wakihamasisha maandamano siku ya Sabasaba wakitaka Serikali ifanye maboresho ya kidemokrasia ikiwemo katiba mpya, kumaliza utekaji na kumwachia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu.
Wanahabari wa Nukta TV na Nukta Habari wameshuhudia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa doria katika sehemu kuu za makutano ya barabara na karibu na miundombinu ya umma.
Sehemu kubwa ya maduka yakiwemo ya Manzese, Magomeni, Banana, Kinondoni, Kimara, Makumbusho, Mbezi Beach, Mwenge na Mabibo yalikuwa hayajafunguliwa hadi majira ya saa 4 asubuhi huku manyunyu yakinyesha katika baadhi ya maeneo.

Si kawaida kwa maeneo haya kushuhudia wafanyabiashara wakichelewa kufungua biashara zao katika siku nyingine za sikukuu au mwisho wa juma. Katika siku za sikukuu kama Sabasaba watumishi wengi wa umma na sekta binafsi huwa katika mapumziko.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wafanyabiashara huwa wanaendelea na shughuli zao kama ilivyo kawaida huku wengine wakikesha kutoa huduma.
Watu wanaendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi licha ya baadhi ya maeneo ya jiji kushuhudia changamoto za usafiri wa umma kutokana na uchache wa magari. Sehemu kubwa ya barabara zina msongamano hafifu kiasi cha kuchukua muda mfupi kufika sehemu inayoenda.
Ulinzi umekuwa ukiimarishwa siku hadi siku kuelekea siku ya leo Julai 7, ambayo ilipangwa kufanyika kwa maandamano.
Serikali imepiga maarufuku maandamano hayo wakiyataja kuwa ni vurugu zisizotambulika kisheria kwa kuwa hayakufuata sheria na taratibu za kuandaa na kufanya maandamano nchini.

Julai 4, 2026, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliwataka wananchi kupuuza wito wowote unaohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani, likisisitiza kuwa halitakuwa tayari kumlinda yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.
Siku moja baadaye, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, aliwaambia wanahabari katika Maonesho ya Sabasaba kuwa kuna baadhi ya wahamasisha wamekamatwa na uchunguzi dhidi yao upo mwishoni ili wachukulie hatua za kisheria. Hakutaja idadi kamili ya waliokamatwa.
Misime alieleza Julai 5 kuwa baadhi ya wanaohamasisha maandamano hao wamepanga kufanya uhalifu mwingine ikiwemo kuwaua viongozi na wananchi, kuchoma shule na kupora mali za umma na watu binafsi.
Hata hivyo, baadhi ya machapisho mtandaoni yalidai kuwa maandamano hayo, yasiyokuwa na kiongozi, yalipangwa kufanyika kwa amani.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi jana aliwataka Watanzania kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi na kwamba Serikali itachukua hatua stahiki kwa yeyote atakayetishia au kufanya uhalifu au kutowesha amani.
“Kwenye kila maeneo tutaendelea kuimarisha ulinzi na usalama ili kuhakikisha kila raia anastahili kwenda kufanya shughuli za uchumi aende, kwenye maeneo ya biashara kama kawaida, kote tupo,” alisema Katambi kwenye mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam.