Huu hapa mwarobaini wa foleni za barabarani Dar

May 20, 2026 5:24 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • ‘Flyover’ 4, barabara 3 kujengwa Dar.
  • Utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na mingineyo uutatumia Sh2.4 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27.

Arusha. Huenda wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakaondokana na adha ya foleni na misongamano ya vyombo vya usafiri barabarani baada ya Serikali kutangaza kuendeleza miradi mikubwa ya barabara, madaraja katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Miongoni mwa maeneo yatakayoguswa na mpango huo ni Jiji la Dar es Salaam, ambalo mara kadhaa limekuwa likishuhudia foleni za mara kwa mara suala linalokwamisha baadhi ya shughuli za kiuchumi.

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni Dodoma leo Mei 20, 2026 amesema lengo la ujenzi wa miundombinu hiyo ni kuboresha maisha ya Wananchi. 

“Tutatumia rasilimali zetu tulizonazo kuhakikisha kwamba ujenzi unafanyika katika namna ambayo hakuna watu watakaoachwa nyuma kimaendeleo kwa sababu ya jiografia, foleni na ukosefu wa ubunifu…lengo ni kuboresha mfumo wa usafiri mijini kuongeza tija ya kiuchumi na kuongeza ubora wa maisha ya Wananchi,” amesema Ulega.

Februari 23 mwaka huu wakati akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Ulega alitangaza dau la Sh10 milioni kwa mwanafunzi atakaye wasilisha andiko lenye suluhu ya changamoto hiyo.

Wiki moja iliyopita wizara hiyo ilimtangaza Tukay Thomas, Mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi UDSM kuwa mshindi katika shindano hilo jambo lilioashiria matumaini ya utatuzi wa foleni nchini.

‘Flyover’ 4, barabara 3 kujengwa Dar

Kwa mujibu wa Ulega, wizara yake imejipanga kukamilisha ujenzi wa barabara tatu za mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), madaraja ya juu (Flyover) manne na upanuzi wa barabara nyingine nne katika mwaka wa fedha 2026/2027 utakaonza Juni.

Barabara zitakazohusishwa ni pamoja na mradi wa BRT awamu ya tatu unaotoka Maktaba Posta hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kupitia Gongo la Mboto wenye urefu wa kilomita 23.3. 

Pia ipo awamu ya nne kutoka Maktaba Posta kuelekea Morocco, Mwenge na Tegeta hadi Ubungo yenye kilomita 30.1, pamoja na awamu ya tano kutoka Ubungo hadi Bandarini na kutoka makutano ya Tabata hadi Segerea pamoja na Tabata hadi Kigogo yenye urefu wa kilomita 27.6.

Serikali pia imesema itaendelea na ujenzi wa madaraja ya juu ya Tabata, Fire, Magomeni, KAMATA na mengine mawili katika makutano ya Mwenge na Morocco ambapo majadiliano yanaendelea na JICA ili kuweza kufadhili utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, katika mwaka huu wa fedha barabara tatu zitapanuliwa ikiwemo barabara ya Ubungo hadi Kimara kutoka njia sita kuwa njia nane, barabara ya Mbagala, Kongowe hadi Mkuranga yenye kilomita 17.14 kutoka njia mbili hadi njia nne  pamoja na Daraja la Mzinga.

“Upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki yenye kilomita 11.77 kutoka njia mbili kuwa njia nne, upanuzi wa barabara ya Kibaha hadi TAMCO yenye kilomita 4.5 kutoka njia mbili hadi njia nane,” amesema Ulega.

Katika hatua nyingine wizara hiyo imetaja ujenzi wa na upanuzi wa miundombinu ya barabara katika Jiji la Arusha, Mbeya, Mwanza, Dodoma Iringa, Songwe na Singida kuwa miongoni mwa vipaumbele ili kuendelea kutatua changamoto hiyo ya msongamano.

Mipango ya  uendelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi wa miundombinu umeifanya Wizara ya Ujenzi kuliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh2.5 trilioni huku asilimia 96 (Sh2.4 trilioni) ikiwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV