Serikali ya Tanzania yatangaza tahadhari, Ebola ikisambaa DRC, Uganda
- Zaidi ya watu 80 wanashukiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza hali ya tahadhari ya kiafya kufuatia kusambaa kwa virusi hatari vya Ebola aina ya (bundibujo) katika ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya visa vipya vya ugonjwa huo kuthibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Katika mahojiano maalumu na Shirika la Habari la Serikali ya China (Xinhua) Mei 17,2026 Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Majanga kutoka Wizara ya Afya Erasto Sylvanus alisema tayari Serikali ya Tanzania imeongeza hatua za kinga na ufuatiliaji katika mipaka, viwanja vya ndege na maeneo mengine ya kuingilia nchini ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
“Kwa kushirikiana na ofisi ya WHO nchini, Tanzania imefanya tathmini ya haraka kubaini maeneo yenye hatari kubwa kutokana na ukaribu na mwingiliano wa watu kati ya Tanzania, Congo na Uganda ili kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za Afya,” amesema Sylvanus.
Tanzania imetangaza tahadhari hiyo ikiwa ni saa chache tangu Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza mlipuko wa Ebola kuwa Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa (PHEIC), kufuatia ongezeko la maambukizi na vifo Mashariki mwa DRC.
Taarifa rasmi zinaonyesha kuwa hadi sasa watu wanane wamethibitishwa kuwa na Ebola katika Jimbo la Ituri huku watu zaidi ya 246 wakishukiwa kuambukizwa ugonjwa huo.
Zaidi ya watu 80 wanaoshukiwa kufariki kutokana na Ebola tayari wameripotiwa katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa DRC, huku maeneo yaliyoathirika zaidi yakitajwa kuwa Bunia, Rwampara na Mongbwalu.
Nchi ya Uganda pia tayari imethibitisha wagonjwa wawili wa Ebola mjini Kampala ndani ya saa 24, ambapo mmoja wao akifariki dunia suala linaloendelea kuibua hofu ya kusambaa kwa ugonjwa huo nchini Tanzania kutokana na kupakana na nchi hizo.

Kuosha mikono ni mionngoni mwa kanuni za kiafya zinazoweza kutumiwa kudhibiti usambaaji wa ugonjwa huo. Picha|Getty Image.
Tahadhari yaimarishwa katika vituo vya afya
Sylvanus amefafanua kuwa Serikali imeweka hospitali zote katika hali ya tahadhari kubwa huku vyumba maalumu vya kuhudumia wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola vikiandaliwa katika vituo vya afya.
“Serikali ya Tanzania imeimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa wenye dalili zinazofanana na Ebola katika jamii na vituo vya kutolea huduma za afya nchini kote na kusambaza miongozo ya kitaalamu kwa mamlaka za mikoa ili kuongeza uwezo wa maandalizi, kinga na mwitikio dhidi ya Ebola,” inaeleza taarifa ya Sylvanus.
Pia timu za wataalamu wa afya kutoka ngazi ya taifa zimepelekwa katika maeneo yenye hatari kubwa huku timu nyingine zikiwa tayari kupelekwa kulingana na mahitaji yatakayojitokeza.
Katika hatua nyingine ya kuimarisha uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo, Maabara ya Taifa ya Afya ya Umma imeelezwa kuwa na uwezo wa kuthibitisha virusi vya Ebola ndani ya saa 24.
Serikali pia tayari imepeleka maabara ya simu katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya uchunguzi wa haraka wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya Ebola.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuna hofu kubwa kuwa kiwango halisi cha maambukizi kinaweza kuwa kikubwa zaidi kutokana na ongezeko la vifo vya ghafla katika jamii pamoja na wagonjwa wanaoripotiwa katika maeneo mbalimbali ya DRC.
“Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu ukubwa halisi wa maambukizi na maeneo ambayo tayari yamefikiwa na virusi hivi,” amesema Tedros.
Tofauti na Ebola aina ya Zaire ambayo tayari ina chanjo na tiba maalumu, hadi sasa hakuna chanjo wala dawa zilizoidhinishwa mahsusi kwa Ebola aina ya Bundibugyo, jambo ambalo limeongeza hofu kuhusu uwezo wa kudhibiti mlipuko huo haraka.
Latest