Wafanyabiashara waonywa kupandisha bei ya vyakula msimu wa Ramadhani, Kwaresma

January 29, 2026 12:58 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Waziri asema akiba ya chakula nchini inajitoshereza.
  • Awahimiza wananchi kutumia chakula kwa uangalifu, kutunza akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewaonywa wafanyabiashara nchini kuacha kutumia miezi ya Ramadhani na Kwaresima kama kisingizio cha kupandisha bei za vyakula suala linaloacha maumivu kwa wananchi.

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba aliyekuwa akizungumza wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni leo Januari 29, 2026 amesisitiza kuwa Taifa lina akiba ya kutosha ya chakula hivyo wafanyabiashara hawapaswi kupandisha bei.

Nitoe rai kwa wafanyabiashara wasitumie vipindi hivi vya Kwaresma na Mwezi mtukufuu wa Ramadhani kujipatia faida iliyopitiliza viwango na kuwaumiza Watanzania kwa kisingizio cha tahadhari ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA),” amesisitiza Waziri Mkuu.

Si mara ya kwanza kwa Serikali kutoa wito kwa wafanyabiashara kuacha kupandisha bei za bidhaa, hususan vyakula, kila inapokaribia miezi ya mifungo ya kidini kama Ramadhani na Kwaresma.

Mifungo hiyo inayotarajiwa kuanza kati ya Februari 17 na 18 kwa Waislamu na baadhi ya Wakristo duniani, inalenga kuwakumbusha waumini umuhimu wa misingi ya imani zao, sambamba na kuhimiza mshikamano na kuwajali watu wenye kipato cha chini.

Tanzania inajitosheleza kwa chakula

Dk Nchemba amekiri uwepo wa ufinyu wa mvua unaochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotangazwa na TMA siku za hivi karibuni akiwahakikishia Watanzania kuwa chakula kipo cha kutosha hivyo hakuna sababu ya kupandisha bei za vyakula.

““Kwa sasa tuna chakula cha kutosha. Mahitaji ya akiba ya chakula kitaifa ni takribani tani 150,000…

…Nchi ina zaidi ya tani 400,000 za akiba. Kati ya hizo, tani 150,000 ni kiwango cha kawaida na zaidi ya tani 200,000 ni ziada,” alisema Waziri Mkuu akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Nancy Hassan Nyalusi.

Kuanzia Septemba 2025 TMA  imekuwa ikiwatahadharisha wananchi juu ya uwezekano wa kunyesha kwa mvua pungufu, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na kusababisha wakulima kuvuna mazao machache kuliko ilivyotarajiwa.Pamoja na uwepo wa changamoto hiyo, Serikali imesema itaendelea kuwahamasisha wakuu wa mikoa na wilaya kutoa elimu kwa wananchi, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache, ili wapande mazao yanayostahimili ukame na yanayoweza kukomaa kwa kutegemea mvua zisizo na mtawanyiko mzuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks