Aweso: Bili za maji zitolewe kulingana na matumizi
- Atoa rai kwa wananchi kulipia kiasi cha maji walichotumia licha kuwepo kwa shida ya maji.
Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Juma Aweso, ameiagiza Mamlaka ya Usambazaji wa Maji na Huduma za Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasa) kuhakikisha wananchi wanalipa bili ya maji kulingana na kiasi halisi walichotumia.
Akijibu swali la mwandishi wa habari leo Januari 28, 2026 alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia ndani ya siku 100, Aweso amesema hali hiyo haivumiliki akitoa agizo kwa Mkurugenzi wa Dawasa kuhakikisha anatatua tatizo hilo.
“Wananchi hawakupata maji ile ipasavyo, itashangaza sana unamwambia mwananchi alipe laki tatu, laki laki tano utadhani vile anakiwanda haiwezekani,” amesema Aweso.
Kauli ya Aweso inakuja kufuatia malalamiko ya mara kwa mara ya watumiaji wa maji nchini kubambikiziwa bili isiyoendana na matumizi halisi hususani wakati wa changamoto ya upatikanaji wa maji iliyojitokeza katika baadhi ya maeneo jiji la Dar es Salaam kuanzia Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa Dawasa, shida hiyo ilitokana na kukauka kwa vyanzo vya maji, hususan Mto Ruvu, ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa jiji hilo huku maeneo yaliyoathirika zaidi yakiwa ni Chamazi, Mabwepande, Bunju, Kunduchi, Vingunguti na baadhi ya maeneo ya Kibamba.
Lipieni kiasi mlichotumia
Aweso amewarai wananchi kulipia kiasi cha maji walichotumia akifafanua kwamba licha ya kuwepo kwa shida ya maji katika baadhi ya maeneo, bado kuna siku ambazo maji yalitoka.
“Na mwananchi nae afahamu kuwa sio kipindi chote katika siku thelathini alikosa maji, kuna kipindi alipata… maji yaliyokuwepo yaligawiwa,” amefafanua Aweso akiwahamasisha wananchi kulipia huduma ya maji.
Kauli ya Aweso inakuja ikiwa ni masaa machache baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, kumwagiza Naibu Waziri wa Maji, Kundo Andreas Mathew kuhakikisha kuwa wizara inalifanyia kazi tatizo hilo na kulitatua katika kipindi cha maswali na majibu bungeni.
“Kulikuwa na uhaba mkubwa sana wa maji Dar es Salaam lakini bili zinaendelea kuja kama kawaida. Shida ni nini?, kalifanyie kazi,” aliagiza Zungu.
Pamoja hayo Serikali pia imebainisha kuwa itakamilisha mradi wa maji Kigamboni unaojumuisha visima virefu, pamoja na Tenki kubwa lenye ujazo wa lita milioni 15 ambao utaupa nguvu mto ruvu kusambaza maji kwa wakazi wa jiji hilo wakati wa kiangazi ili kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji.
Latest