WHO yatoa mwongozo mpya wa lishe mashuleni kudhibiti unene uliopitiliza

January 28, 2026 4:45 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Takribani watoto na vijana milioni 188 wa umri wa kwenda shule waliishi na unene uliopitiliza 2025.
  • Ni nchi 48 pekee kati ya 408 zilizo na sera zinazozuia matangazo ya vyakula visivyofaa kwa watoto.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo mpya wa kimataifa wa lishe mashuleni, unaoziitaka nchi wanachama kuimarisha mazingira ya lishe shuleni ili kudhibiti ongezeko la unene uliopitiliza na kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa watoto.

Uzito au unene uliopitiliza hufafanuliwa kama mkusanyiko usio wa kawaida au wa kupita kiasi wa mafuta mwilini ambao unaweza kuweka afya hatarini ikichangiwa zaidi na mtindo mbovu wa maisha, ulaji usiozingatia kanuni za afya na tabia bwete.

Takwimu za WHO zinakadiria kuwa mwaka 2024 takribani watoto milioni 35 walio chini ya umri wa miaka mitano duniani kote walikuwa na uzito uliopitiliza suala linaloweka afya zao rehani.

Hali ni mbaya zaidi kwa watoto na vijana milioni 188 wenye umri wa kwenda shule ambao waliripotiwa na WHO kuwa na unene uliopitiliza, sawa na mtoto mmoja kati ya 10, idadi iliyozidi kwa mara ya kwanza watoto wenye uzito pungufu.

WHO inapendekeza shule ziweke kanuni za lazima zitakazohamasisha upatikanaji wa vyakula vyenye afya. Picha/Canva.

Kutokana na uwepo wa changamoto hiyo, January 27, 2026, WHO ilitoa mwongozo wa lishe mashuleni utakaohakikisha vyakula na vinywaji vinavyotolewa shuleni, pamoja na vinavyopatikana katika mazingira yanayozunguka shule, ni vyenye afya na lishe bora.

“Uzito kupita kiasi na unene uliokithiri kwa watoto vinaendelea kuongezeka duniani, huku utapiamlo bado ukiwa changamoto ya kudumu. Shule ziko mstari wa mbele katika kukabiliana na mzigo huu maradufu wa utapiamlo,” inaeleza sehemu ya taarifa ya WHO.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus aliyekuwa akizunngumza alisema kuwa lishe shuleni ina athari ya moja kwa moja katika afya na maendeleo ya watoto.

“Chakula ambacho watoto hula shuleni kinaweza kuathiri uwezo wao wa kujifunza na kuwa na madhara ya muda mrefu kwa afya na ustawi wao. Lishe sahihi shuleni ni msingi wa kuzuia magonjwa baadaye maishani,” alisema.

Takribani mtoto mmoja kati ya 10 duniani ana unene uliopitiliza. Shule zinaweza kuwa sehemu ya kutatua tatizo hili. Picha/ Canva.

Katika muktadha wa kitaifa, baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania, tayari zina miongozo ya chakula cha shule inayolenga kuboresha lishe kwa wanafunzi kupitia Mpango wa Taifa wa Chakula Shuleni (NSFG).

Mpango huo unazingatia Sera ya Afya ya mwaka 2007, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Taifa wa Sekta Jumuishi wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Lishe 2016/17 hadi 2020/2.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, utoaji wa huduma za chakula shuleni huchangia kuboresha afya ya wanafunzi, kupunguza utoro, kuongeza usikivu darasani na kuinua kiwango cha ufaulu.

WHO inakadiria kuwa zaidi ya watoto milioni 466 duniani hupata chakula kupitia programu za chakula shuleni jambo linaloimarisha afya ya akili na kuimarisha uwezo wao wa kimasomo.

Kuongeza vyakula vyenye afya na kupunguza vyenye sukari na mafuta yasiyo na afya ni hatua muhimu ya kuwalinda watoto. Picha/ Canva.

Hata hivyo, shirika hilo linaonya kuwa bado kuna upungufu wa taarifa kuhusu ubora wa lishe ya chakula hicho, hali inayoweza kusababisha changamoto za kiafya.

Katika mwongozo wake mpya, WHO inapendekeza shule ziweke kanuni za lazima zitakazohamasisha upatikanaji wa vyakula vyenye afya na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi na mafuta yasiyo na afya, pamoja na kudhibiti mbinu za kibiashara zinazowalenga watoto.

Kwa sasa, nchi 104 zina sera za chakula chenye afya mashuleni huku karibu robo tatu zikiwa na vigezo vya lazima vya kuongoza muundo wa chakula cha shule huku nchi 48 pekee zikizuia matangazo ya vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi au mafuta yasiyo na afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks