NMB yazalisha zaidi ya ajira 2,470 ndani ya miaka mitano

January 28, 2026 3:00 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaajiri wataalamu zaidi ya 80 wa teknolojia, takwimu (data) na usalama wa mifumo.

Dar es Salaam. Benki ya NMB imesema imezalisha ajira zaidi ya 2,470 za moja kwa moja ndani ya kipindi cha miaka mitano, huku idadi ya wafanyakazi ikifikia 5,762 mwaka 2025 hatua inayotajwa kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira na kukuza uchumi wa Watanzania.

Mkurugenzi Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Ruth Zaipuna, aliyekuwa akizungumza leo Januari 28, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuhitimisha Mpango Kazi wa miaka mitano wa 2021/25 na kuzindua Mpango Kazi mpya wa 2026/30 amesema benki hiyo imepiga hatua kubwa katika kukuza rasilimali watu na kutoa fursa za ajira.

“Benki hii imezalisha ajira za moja kwa moja 2,470, mwaka 2000 Benki ya NMB tulikuwa na jumla ya wafanyakazi 3,929, tumemaliza mwaka 2025 tukiwa na jumla ya wafanyakazi 5,762 wale wa kudumu na wale wafanyakazi wa muda wa kati,” anaeleza Zaipuna.

Kwa upande wa uwekezaji wa kimkakati, Zaipuna amesema benki hiyo imewekeza zaidi ya Sh230 bilioni katika mifumo ya kibenki na teknolojia ya kisasa ndani ya kipindi hicho. 

Miongoni mwa mwa watalaamu 80 walioajiliwa jukumu lao ni kuendesha mifumo ya kibenki. Picha/CBN.

Uwekezaji huo umeiwezesha NMB kuajiri wataalamu zaidi ya 80 wa teknolojia, takwimu (data) na usalama wa mifumo, hatua iliyochangia kuimarisha ajira za kitaalamu katika sekta ya fedha.

Ameongeza kuwa uwekezaji unaoendelea katika teknolojia na rasilimali watu umeiwezesha benki kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia huduma za kifedha, sambamba na utekelezaji wa mikakati ya ujumuishaji wa kifedha na upanuzi wa huduma katika maeneo ya mijini na vijijini.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema Serikali inaifuatilia Benki ya NMB kwa karibu kutokana na uwekezaji mkubwa ilio nao.

“Tunawawekezaji wa kimkakati wakubwa wawili ambao wote tuna zaidi ya asilimia 30, kwa hiyo jicho letu tunaliweka kwa karibu sana na hiyo pia inatakiwa ilete imani kubwa hata kuwawekezaji wengine ,” amesema Mchechu.

Mchechu ameongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda maslahi ya benki hiyo na wawekezaji wake kwa kuhakikisha bodi na uongozi vinaendelea kuwa imara na makini katika kusimamia ukuaji wa taasisi hiyo ya kifedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks