Grok yageukia mfumo wa malipo, mataifa waikosoa
- Ni kufuatia malalamiko makubwa kuhusu matumizi mabaya ya teknolojia hiyo kutengeneza picha za utupu za wanawake na watoto.
Dar es Salaam. Chatbot ya Akili Mnemba (AI) Grok, imeripotiwa kugeukia mfumo wa malipo utakaozuia watumiaji wasiokuwa na alama ya uthibitisho (blue tick) katika mtandao wa kijamii wa X kushindwa kuhariri na kuunda picha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 10, 2026 kupitia mtandao wa X, Grok inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Elon Musk itapatikana kwa watumiaji waliolipia pekee suala linalotajwa kupunguza uzalishaji wa maudhui yasiyofaa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Grok kukosolewa vikali kwa kudaiwa kutumika kuunda picha za utupu za wanawake na watoto, hali iliyozua taharuki kimataifa na kumuweka Musk katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo faini.
Uamuzi wa kufanya huduma hiyo kuwa ya kulipia utawalazimu watumiaji wanaotaka kuendelea kutumia huduma hizo kuwasilisha taarifa zao binafsi pamoja na taarifa za kadi za malipo jambo litakalopunguza uundaji wa picha hizo zisizo na maadili.

Mataifa yakosoa uamuzi huo
Pamoja na muelekeo huo mpya wa Grok, viongozi wa kimataifa ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer imepinga vikali uamuzi huo ikidai hatua hiyo si suluhisho.
“Kugeuza huduma inayoweza kutengeneza maudhui yasiyo halali kuwa ya kulipia ni dharau kwa waathiriwa wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia,” imesema Keir Starmer.
Kwa upande wa Umoja wa Ulaya (EU), msemaji wa masuala ya kidijitali Thomas Regnier amesema ni wajibu wa majukwaa husika ikiwemo X kuhakikisha yanazuia kabisa uzalishaji wa maudhui haramu.
EU pia imeiagiza X kuhifadhi nyaraka na data zote zinazohusiana na Grok hadi mwisho wa mwaka 2026 kutokana na sakata hilo.

Nchi nyingine zikiwemo Ufaransa, Malaysia na India pia zimeikosoa X kwa kushindwa kudhibiti matumizi ya Grok, huku zikitoa wito wa kuwepo kwa udhibiti madhubuti wa teknolojia za AI.
Pamoja na ukosoji huo, Musk ametangaza kuwa mtu yeyote atakayemtumia Grok kutengeneza maudhui ya kinyume cha sheria atachukuliwa hatua sawa na anayechapisha maudhui hayo moja kwa moja mtandaoni.
Latest