Fahamu wanamichezo 10 wanaolipwa zaidi duniani 2025

December 29, 2025 5:42 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Michezo hiyo ni pamoja na soka, mpira wa kikapu, gofu, pamoja na mpira wa miguu wa marekani NFL.
  • Cristiano Ronaldo ndiye mwanamichezo anaelipwa pesa nyingi zaidi duniani akiwa na mapato ya jumla ya Dola za Marekani milioni 260.

Dar es salaam. Katika dunia iliyosheheni vipaji na michezo mbalimbali kama soka, mpira wa kikapu na gofu kuna wanamichezo wachache waliofanikiwa kugeuza vipaji vyao kuwa vyanzo vikubwa vya utajiri. 

Wakiwa na uwezo wa kipekee uwanjani na ushawishi mkubwa nje ya uwanja, nyota hawa hujiizolea mamilioni ya fedha kupitia mishahara, bonasi, na mikataba minono ya udhamini.

Kwa mujibu wa Jukwaa la Takwimu la WorldStats, Nukta Habari imekuchambulia orodha ya wanamichezo 10 waliolipwa pesa nyingi zaidi duniani kwa mwaka 2025. 

10. Lamar Jackson 

Lamar Jackson, ni nyota wa timu ya mpira wa miguu wa Marekani Baltimore Ravens, Jackson anashikilia nafasi ya kumi katika orodha hii akikadiriwa kuingiza mapato ya Dola za Marekani milioni 100.5 sawa na Sh265 bilioni. 

Kiasi kikubwa cha mapato ya Jackson kinatokana na mkataba wake mnono na timu ya  Ravens, huku kiasi cha Dola za Marekani milioni 2 (sawa na Sh5.28 bilioni) zikichangiwa na mikataba ya udhamini. 

Kiwango hicho cha fedha kinamfanya Jackson kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika Ligi ya Mpira wa Miguu wa Marekani (NFL).

Lamar Jackson ndiye mchezaji anayelipwa zaidi katika Ligi ya Mpira wa Miguu wa Marekani (NFL). Picha | Britanica.

9. Stephen Curry

Stephen Curry, nahodha wa timu ya mpira wa kikapu ya Golden State Warriors, kwa mwaka 2025 anakadiriwa kuingiza jumla ya Dola za Marekani milioni 102 sawa na Sh269.5 milioni kwa mwaka 2025. 

Akiwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA), Curry anapokea kiasi cha Dola za Marekani milioni 52 sawa na Sh137.43 bilioni kama mshahara wake.

Mbali na mpunga huo anaoingiza kupitia mpira wa kikapu, Curry anaingiza Dola za Marekani Milioni 50  (sawa na Sh132.15 bilioni.) kupitia biashara zake anazozifanya nje ya uwanja.

8. Karim Benzema 

Baada ya kuondoka Real Madrid na kujiunga na Al-Ittihad ya Saudi Arabia, nyota wa mpira wa miguu kutokea Ufaransa, Karim Benzema ameongeza mapato yake kufikia kiasi cha Dola za Marekani milioni 106 sawa na Sh280.15 bilioni. 

Mapato hayo yana jumuisha Dola za Marekani milioni 100 sawa na Sh264.3 bilioni kutoka kwenye mshahara na bonasi zake za uchezaji, huku Dola za Marekani milioni 6 sawa na Sh15.858 bilioni zikitokana na mikataba ya udhamini.

Jon Rahm nyota wa mpira wa Gofu kutokea Uhispania amevunja rekodi ya mapato kwenye mchezo wa gofu 2025, anakadiriwa kukusanya jumla ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 218 sawa na Sh576.17 bilioni. Picha | CNN.

7. Neymar

Nyota wa mpira wa miguu kutokea Brazil, Neymar, anakadiriwa kujikusanyia kiasi cha Dola za Marekani milioni 108 sawa na Sh285.444 bilioni kwa mwaka 2025, kiasi kikubwa cha mapato ya Neymar kimetokana na mkataba wake na klabu ya  Al-Hilal kutokea nchini Saudi Arabia. 

Mapato yake ya uwanjani yamefikia kiasi cha Dola za Marekani milioni 80 sawa na Sh211.44 bilioni, huku mikataba ya udhamini na makampuni makubwa kama Puma na Red Bull ikimletea Dola za Marekani milioni 28 sawa na Sh74 bilioni

6. Kylian Mbappe 

Nyota wa mpira wa miguu kutokea Ufaransa Mbappe, ni mmoja wa wachezaji vijana wenye vipaji vikubwa katika soka, Mbappe anakadiriwa kuingiza mapato ya Dola za Marekani milioni 110 sawa na Sh290.73 bilioni, kwa mwaka 2025. 

Kati ya hizo, kiasi cha Dola za Marekani milioni 90 sawa na Sh237.87 bilioni kinatokana na mshahara wake katika klabu ya Real Madrid na timu ya Taifa ya Ufaransa, huku kiasi cha Dola za Marekani milioni 20 sawa na Sh52.86 bilioni zikitokana na mikataba ya udhamini na makampuni kama Nike na EA Sports.

Mbappe anakadiriwa kuingiza mapato ya Dola za Marekani milioni 110 sawa na Sh290.73 bilioni, kwa mwaka 2025. Picha | Britannica.

5. Giannis Antetokounmpo 

Nyota raia wa Ugiriki, Giannis Antetokounmpo, maarufu kama ‘Greek Freak’  ni nyota anaeendelea kutawala Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) kwa umahiri mkubwa akikadiriwa kukusanya kiasi cha Dola za Marekani milioni 111 sawa na Sh293.373 bilioni kwa mwaka 2025. 

Mshahara wake kutoka timu yake ya Milwaukee Bucks unamuingizia kiasi cha Dola za Marekani milioni 46 sawa na Sh121.578 bilioni, huku mikataba yake ya kibiashara, ikimwingizia kiasi cha Dola za Marekani milioni 65 zaidi sawa na Sh171.795 bilioni. 

4. LeBron James 

LeBron James, sio tu gwiji wa mpira huo katika Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini humo (NBA) bali pia mfanyabiashara mahiri anayekadiriwa kuingizaa Dola za Marekani milioni 128.2 sawa na Sh338 bilioni, 

Kati ya fedha hizo, Dola za Marekani milioni 48.2 sawa na Sh127.44 bilioni zinatoka kwenye mshahara wake katika timu ya mpira wa kikapu ya LA Lakers, na Dola za Marekani milioni 80 sawa na Sh211.44 ni kutoka kwenye uwekezaji wake katika biashara kama Blaze Pizza na kampuni yake ya SpringHill Entertainment. 

Lebron James ndiye mchezaji wa mpira wa kikapu anayelipwa zaidi kwa mwaka 2025. Picha | ESPN

3. Lionel Messi 

Lionel Messi, nyota wa mpira wa miguu kutoka Ajentina na bingwa wa Kombe la Dunia 2022, ni moja kati ya wachezaji wa soka wa muda wote anayechezea klabu ya Inter Miami iliyoko Marekani. 

Kwa mwaka 2025 Messi amekadiriwa kuingiza kiasi cha Dola za Marekani 135 milioni sawa na Sh355.805 bilioni, ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 65 sawa na Sh171.795 bilioni zinatoka kwenye mshahara wake klabuni hapo, huku Dola za Marekani milioni 70 sawa na Sh184.01 bilioni zikitoka kwenye mikataba yake na makampuni makubwa kama Adidas, Pepsi, na Budweiser. 

2. Jon Rahm 

Jon Rahm nyota wa mpira wa Gofu kutokea Uhispania amevunja rekodi ya mapato kwenye mchezo wa gofu 2025, anakadiriwa kukusanya jumla ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 218 sawa na Sh576.17 bilioni. 

Kiasi kikubwa cha mapato ya Rahm, Dola za Marekani milioni 198 sawa na Sh519.414 bilioni ni kutokana na uchezaji wake katika ligi ya LIV Golf, huku Dola za Marekani milioni 20 sawa na Sh52.86 bilioni zikichangiwa na mikataba ya udhamini na makampuni kama Callaway na Rolex. 

Cristiano Ronaldo ndiye mwanamichezo anaelipwa pesa nyingi zaidi duniani akiwa na mapato ya jumla ya Dola za Marekani milioni 260. Picha | BBC

1. Cristiano Ronaldo 

Kwa mara nyingine tena, Nyota na mchezaji bora wa mpira wa miguu wa muda wote, Cristiano Ronaldo anaongoza orodha ya wanamichezo waliolipwa zaidi duniani kwa mwaka 2025 akikadiriwa kukusanya mapato ya jumla ya Dola za Marekani milioni 260 sawa na Sh681.18 bilioni. 

Uhamisho wake kwenda klabu ya mpira wa miguu ya Al-Nassr umeongeza mshahara wake hadi kufikia Dola za Marekani milioni 200 sawa na Sh528.6 bilioni kwa mwaka, kiwango cha juu zaidi kwa mwanamichezo yeyote ulimwenguni. 

Mbali na soka, Ronaldo anaingiza kiasi cha Dola za Marekani milioni 60 sawa na Sh158.58 bilioni kupitia biashara zake binafsi kama chapa yake ya CR7 na mikataba ya udhamini na makampuni makubwa kama Nike na Herbalife. Ronaldo si tu nyota wa soka, bali pia nembo ya biashara inayovutia mashabiki na wadau wa michezo kote duniani. 

Cristiano Ronaldo pia ndiye binadamu mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii akifikisha wafuasi zaidi ya bilioni moja, Jukwaa la Michezo la Sportico limeripoti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks