Uhamiaji yatangaza nafasi za ajira kwa vijana Tanzania
- Fani zitakazopewa kipaumbele ni pamoja na lugha za kimataifa, utawala, sheria, uhusiano, TEHAMA, uchumi, uhasibu, ununuzi na ugavi
Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji Tanzania imetangaza nafasi za ajira kwa vijana wa kitanzania wenye elimu na ujuzi katika fani mbalimbali, likiwataka kutuma maombi yao kupitia mfumo wa ajira wa jeshi hilo kabla ya Januari 12, 2026.
Taarifa ya Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Daniel Kyauri iliyotolewa leo Desemba 29, 2025 inabainisha kuwa ajira hizo ni kwa ajili ya vijana wenye elimu ya kidato cha nne na ujuzi katika fani mbalimbali kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada.
Miongoni mwa sifa zilizoanishwa na jeshi hilo ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania kuwa na kitambulisho cha uraia au namba ya utaifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Pamoja na sifa hiyo ya msingi taarifa ya Kyauri imebainisha muombaji asiwe amewahi kuajiriwa Serikalini, kwa mwombaji wa elimu ya kidato cha nne awe amepata daraja la kwanza hadi tatu akiwa na umri kati ya miaka 18 hadi 22.
Kwa wahitimu wa Astashahada na Stashahada awe na umri kati ya miaka 18 hadi 25, huku Mwombaji wa Shahada na Stashahada ya Juu awe na umri kati ya miaka 18 hadi 30, wote wakiwa na cheti cha kuzaliwa.
“Muombaji awe na siha na afya njema ya mwili na akili iliyothibitishwa na Daktari wa Serikali, asiwe ameoa/kuolewa na asiwe na mtoto, asiwe na alama au michoro yoyote katika mwili wake (tattoo), awe na nidhamu na tabia njema na awe hajawahi kupatikana na hatia kwa shitaka la jinai mahakamani na hajawahi kufungwa.
… Awe tayari kuhudhuria mafunzo ya awali ya askari magereza na kufanya kazi mahali popote Tanzania bara, awe tayari kujigharamia yeye binafsi katika hatua zote za awali za usaili wa ajira hii hadi kuripoti mafunzoni,” imesema taarifa ya Kyauri.
Fani zitakazopewa kipaumbele
Aidha, Jeshi hilo limeanisha fani ziakazopewa kipaumbele katika utolewaji wa ajira hizo kuwa ni lugha za kimataifa, utawala, sheria, uhusiano, TEHAMA (Cyber Security, Database Developer, System Developer, Artifical Intelligence and Machine Learning).
Fani nyingine ni masijala, ukatibu mahsusi, uhasibu, ununuzi na ugavi waliosajiliwa na bodi, takwimu, uchumi, umeme, ufundi wa AC, Brass band, wataalamu wa saikolojia (Psychology) na mpiga chapa (Printer).
Pia waombaji wenye ujuzi wa ufundi wa magari na udereva watapewa kipaumbele.
Jinsi ya kutuma maombi
Idara ya Uhamiaji imesema maombi yote yafanyike kupitia tovuti ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni https://www.immigration.go.tz kuanzia tarehe 29 Desemba, 2025 na mwisho wa kufanya maombi ni tarehe 11 Januari, 2026.
Wakati wa kufanya maombi, mwombaji anatakiwa kuambatisha (upload) kwenye mfumo wa ajira nyaraka zilizo katika mfumo wa PDF (kila nyaraka moja isizidi 300Kb)
Nyaraka hizo ni pamoja na picha (passport size) iliyopigwa hivi karibuni iliyo katika mfumo wa jpg au png, barua ya maombi ya ajira iliyoandikwa kwa mkono, barua ya utambulisho toka Serikali ya Mtaa au Kijiji.
Kwa walioko kwenye kambi za JKT au JKU wawe na barua za utambulisho kutoka kwa mkuu wa kambi, mwombaji anatakiwa kuambatanisha pia Cheti cha kuzaliwa, Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au namba ya NIDA kwa ajili ya kujisajili kwenye mfumo;
Pia awe na Index namba za vyeti vya kufaulu kidato cha nne na kidato cha sita ambazo atajaza kwenye mfumo wa ajira pamoja na namba ya utambuzi ya cheti cha ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada/Stashahada ya juu inayotambuliwa na TCU au NACTVET.
Idara imeeleza kuwa mwombaji yeyote atakayewasilisha nyaraka za uongo/kughushi (Forged Documents) au kuficha sifa halisi ya elimu atakuwa ametenda kosa la jinai hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Latest