Rais Samia azindua Bunge, ataja vipaumbele vya awamu ya pili ya uongozi
- Ataja kufungua fursa kwa vijana, kuboresha utawala bora na kuimarisha umoja na mshikamano wa Taifa.
- Amuagiza DPP kuwafutia mashtaka walioandamana Oktoba 29.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo amezindua rasmi Bunge la 13 ambapo ametaja vipaumbele vya Serikali katika awamu ya pili ya uongozi wake, ikiwemo kutengenza programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii, na kuwajengea Watanzania kesho iliyo bora zaidi.
Rais Samia ameyabainisha hayo alipokuwa akifungua rasmi Bunge la 13 kwa mara ya kwanza leo Novemba 14, 2025 jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa katika kipaumbele cha kuwafikia vijana Serikali yake iitaboresha ushiriki wa kundi hilo katika masuala ya Maendeleo yao kwa kuanzisha wizara mahususi kwa ajili ya masuala ya vijana.
“Mimi na wenzangu tumefikiria kuwa na Wizara kamili itakayoshughulikia mambo ya vijana, tumeamua kuwa na Wizara kamili badala ya kuwa na Idara iliyo na mambo mengi, vilevile nafikiria kuwa na washauri wa mausala ya vijana ndani ya Ofisi ya Rais” ameongeza Rais Samia.
Aidha, vipaumbele vingine alivyotaja Rais ni pamoja na kuchukua hatua za kuongeza mitaji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za vijana na wanawake kwa kutenga Sh200 bilioni.
Hata hivyo, Rais Samia amesema tayari Serikali yake imetangaza nafasi za ajira 7,000 za walimu na nafasi za ajira 5,000 za watumishi wa afya ili kujibu kiu ya wananchi ya kuboresha huduma za afya na elimu.
Katika kuboresha afya za Watanzania, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kusimamia mpango wa bima ya afya kwa wote kupitia Wizara ya Afya, ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi huku akisistiza kuwa vituo vya kutolea huduma za afya kutozuia kutoa maiti wakati familia zinafuatilia taratibu za kulipa madeni ya matibabu.
Akizungumzia sekta ya usafirishaji, Rais Samia amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itasimamia mpango wa kuwa na waendeshaji binafsi wa reli mpya zinazojengwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambapo hatua ya mwanzo itahusisha Reli ya Tazara.
Vipaumbele vingine ni kuendeleza kazi ya kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuweka mkazo katika kuimarisha utumishi wa umma na utawala bora.
Sanjari na vipaumbele hivyo, Rais amewataka mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na maafisa tarafa kusogea karibu na wananchi ili kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo unakwenda kwa kasi.
Maandamano Oktoba 29 kuchunguzwa
Rais Samia amesema Serikali yake itaunda tume maalumu ya kuchunguza vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 ili kujua kiini cha tatizo hilo.
Vurugu hizo zilizosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa miundombinu mali za umma na binafsi pia zilisababisha kusimamishwa kwa shughuli mbalimbali.
Rais huyo ameeleza kusikitishwa kwake na kilichotokea siku hiyo huku akiwataka wabunge na wageni waliokusanyika bungeni hapo kusimama kwa dakika moja kuwaombea waliopoteza maisha.
Waliokamatwa waachiwe
Aidhaa, Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali DPP, kuwafutia makosa vijana wote walioonekana kushiriki maandamano yaliyosababisha vurugu Oktoba 29, mwaka huu, kwa kufuata mkumbo, akisema baadhi yao hawakujua wanachokifanya.
“Natambua kuna vijana wengi wamekamatwa kwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya na wengine wamefuata mkumbo, nikiwa kama mama navielekeza vyombo vya kisheria kuangalia makosa yaliyofanywa na vijana wetu.
…Kwa wale ambao walifanya mambo kwa kufuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao,” ameeleza Rais Samia.
Latest