INEC yatangaza ratiba mpya uchaguzi ubunge jimbo la Siha
- Taarifa hii inakuja ikiwa zimebaki siku 16 kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
- Uteuzi wa wagombea utahusisha mgombea wa CUF pekee na hautawahusu wagombea wengine.
Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba mpya ya uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Siha, mkoa wa Kilimanjaro.
Uamuzi huo umetokana na kifo cha aliyekuwa mgombea wa ubunge kupitia Chama cha The Civic United Front (CUF) marehemu Daudi Wilibrod Ntuyehabi, kilichotokea Oktoba 8, 2025.
Taarifa hiyo, iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, imeeleza kuwa Tume ilipokea taarifa rasmi kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Siha kuhusu kifo cha Ntuyehabi na kwa mujibu wa kifungu cha 71(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uchaguzi katika jimbo hilo ulisitishwa rasmi Oktoba 8, 2025.
“Uchaguzi katika Jimbo hilo ulisitishwa rasm Oktoba 8, 2025, hivyo, shughuli zote ikiwemo kampeni za uchaguzi wa Ubunge kwa wagombea wengine zimesitishwa katika jimbo tajwa.,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, kwa mujibu wa vifungu vya 68(1), (3), (4) na 71(2) vya sheria hiyo, INEC imetangaza ratiba mpya ya uchaguzi wa Ubunge Jimbo la Siha.
Kulingana na taarifa hiyo Oktoba 15,2025 hadi Oktoba 21,2025 fomu za uteuzi zitatolewa kwa mgombea ubunge jimbo la Siha kupitia CUF.
Siku hiyo hiyo ya Oktoba 21, kutafanyika uteuzi wa mgombea ubunge kupitia chama hicho.
Kampeni za uchaguzi wa ubunge jimbo hilo zitafanyika kuanzia Oktoba 22, 2025 hadi Oktoba 27, 2025 na kusitishwa Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025 ili kupisha siku ya kupiga kura hadi kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Baada ya uchaguzi kampeni zitaendelea tena Novemba 5, 2025 hadi Desemba 29, 2025 na uchaguzi kufanyika siku ya Jumanne Desemba 30, 2025.
Hata hivyo, tume imefafanua kuwa uteuzi mpya utahusisha mgombea wa CUF pekee na hautawahusu wagombea wengine waliokuwa wameteuliwa awali, isipokuwa wale watakaotoa taarifa rasmi ya kujitoa.
Aidha, Tume imezikumbusha taasisi za kisiasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuzingatia Katiba ya Tanzania, sheria za uchaguzi, kanuni, maadili, taratibu, miongozo na maelekezo ya tume, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi na haki.
Taarifa hii ya INEC inakuja ikiwa zimebaki siku 16 pekee kuelekea siku ambayo kampeni za uchaguzi mkuu zitahitimishwa na zoezi la upigaji kura kuchukua nafasi yake.
Kati ya vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa nchini ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pekee ambacho hakitoshiriki uchaguzi wa mwaka huu, ambapo kati ya vyama vinavyoshiriki 17 vimesimamisha wagombea wa urais.
Latest



