Si kweli: Mchanganyiko wa tango na asali ni sumu

October 6, 2025 6:13 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wa lishe wanasema kuwa hakuna ukweli wowote na badala yake tango na asali vina virutubisho muhimu kwa afya ya  mwili wa binadamu. 

Dar es Salaam. Huenda ukawa ni miongoni mwa watu waliowahi kusikia au kuaminishwa kwamba matumizi ya mchanganyiko wa asali na tango hutengeneza sumu na kusababisha kifo.

Dhana hii inayoishi miongoni mwa jamii huwafanya baadhi ya watu kushindwa kutumia tunda hilo na asali kwa pamoja kwa kuhofia kifo suala ambalo halina ukweli wowote.

Utafiti uliofanywa na NuktaFakti kwa kufanya mahojiano na wataalamu wa afya pamoja na majarida ya kisayansi umebaini kuwa taarifa hizo ni za uzushi.

Ukweli ni huu

Mtaalamu wa Lishe, Mwamvua Zuber ameiambia NuktaFakti kuwa hakuna ukweli wowote kuwa mtu anapotumia mchanganyiko wa asali na tango atakufa badala yake amebanisha kuwa vyote ni vitu vyenye virutubisho muhimu katika lishe. 

“Asali inatengenezwa na nyuki na ina mchanganyiko wa vitu vingi sana ikiwemo sukari ambavyo ni muhimu na inasaidia sana katika kuupa mwili nguvu” ameeleza Zuberi.

Wataalamu zaidi wa lishe wanaeleza kuwa dhana hiyo imekuwa ikisambaa baina ya watu pasipo na ushahidi wowote wa kitaalamu katika lishe.

Wataalamu wa lishe wanasema kuwa hakuna ukweli wowote na badala yake tango na asali vina virutubisho muhimu kwa afya ya  mwili wa binadamu. 

Mtaalamu mwingine wa lishe, Irene Kweka amesema kuwa si kweli mtu anapotumia mchanganyiko wa tango na asali anakufa akilitaja tango kama tunda la kipekee ambalo lina umuhimu mkubwa kwa matumizi kwa watu ambao wanahitaji kudhibiti uzito wao.

“Tango ni tunda ambalo lina uchache wa kalori na asilimia kubwa ya maji, hivyo ni nzuri kwa mtu anaehitaji kudhibiti uzito,” ameeleza Kweka. 

Mapitio zaidi ya tafiti za lishe yaliyofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Harvard (Harvard School of Public Health) yanaonyesha kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa mchanganyiko wa asali na tango una sumu au unaweza kusababisha kifo kwa binadamu. 

Kinyume chake, watafiti hao wanasema vyakula hivyo viwili vina virutubisho muhimu kwa mwili, ikiwemo vitamini, madini na antioxidants zinazosaidia kuimarisha kinga na afya ya ngozi. 

Asali imeelezwa kuwa na sifa za antibakteria na kuponya majeraha, huku tango likitajwa kuwa na maji mengi na madini ya potassium yanayosaidia kudhibiti shinikizo la damu. 

Hata hivyo, wataalamu wanashauri watu wenye mzio wa vyakula hivyo watumie kwa tahadhari, kwani athari hutokana na mwitikio wa mtu mmoja mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks