Rais Samia atengua, ateua viongozi wapya DART, UDART

October 2, 2025 1:01 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Amemteua Said Habibu Tunda kuwa Mtendaji Mkuu wa wakala wa DART na Pius Andrew Ng’ingo kuwa Mkurugenzi Mkuu 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametengua na kuteua viongozi wapya akiwemo Mtendaji Mkuu wa wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).

Mabadiliko hayo yanakuja wakati ambao wananchi jijini Dar es Salaam wamekuwa  wakilalamikia huduma zisizoridhisha kwenye usafiri wa mabasi ya mwendokasi.

Mathalani, Jana Jumatano, Oktoba 1, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alifanya ziara ya kushtukiza kwenye kituo cha Kimara, kujionea kero na usumbufu wanaokutana nao abiria hasa nyakati za asubuhi ambapo aliwaomba radhi wakazi wa jiji hilo kutokana na adha ya usafiri.

Kwa muda mrefu usafiri huo umekuwa na changamoto nyingi kiasi cha abiria kulazimika kujazana kwenye vituo na kugombea magari yanapofika vituoni hasa Kimara na Kivukoni.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Oktoba 2, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, imeeleza kuwa, Rais Samia amemteua Said Tunda kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Tunda anachukua nafasi ya Dk Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake umetenguliwa kuanzia leo Oktoba 2, 2025.

Aidha, Rais Samia amemteua Pius Ng’ingo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), akichukua nafasi ya Waziri Kindamba, ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa. 

Taarifa ya uteuzi na utenguzi huo imetolewa wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifanya ziara kwenye kituo cha mwendokasi cha Kivukoni na baadaye Kimara leo.

Hata hivyo, jana Oktoba Mosi 2025, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, iliripoti tukio la kushambuliwa kwa mawe baadhi ya mabasi katika vituo vya mwendokasi katika maeneo ya Gerezani Kariakoo, Magomeni Mapipa, Magomeni Usalama na Magomeni Kagera kutokana na abiria kuchoshwa na kero ya kusuasua kwa huduma za usafiri huo maarufu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, katika tukio hilo watu watatu wanashikiliwa kwa mahojiano huku jeshi likitangaza kuwatafuta wengine waliohusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks