TCRA yaifungia Jamii Forums kwa siku 90
- Ni kutokana na kuchapisha maudhui kinyume na sheria.
Arusha. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesitisha leseni ya kuchapisha maudhui mtandaoni ya kampuni ya Vapper Tech Limited (JamiiForums) na kuzuia upatikanaji wa jukwaa la Jamii Forums kwa siku 90.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabiri Bakari, iliyotolewa leo Septemba 9, 2025 inabainisha kuwa leseni hiyo imesitishwa kutokana na kuchapisha maudhui kinyume na sheria bila kubainisha maudhui yenyewe.
“Mnamo tarehe 04 Septemba 2025, Jamii Forums kupitia jukwaa lake na akaunti zake za mitandao ya kijamii ilichapisha maudhui ya kupotosha Umma, kukashifu na kudhalilisha Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na Marekebisho yake ya mwaka 2022 па 2025,” imesema taarifa ya Dk Bakari.
TCRA imebainisha kuwa maudhui hayo pia yanakinzana na utamaduni, mila na desturi za Kitanzania, jambo ambalo linaathiri umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, na kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Jamii Forums uamuzi wa TCRA umetokana na wao kuchapisha taarifa ya mwanasiasa Humphrey Polepole kuhusu mfanyabiashara Rostam kumiliki mgodi wa makaa ya mawe kwa asilimia 70 na taarifa za uhusiano kati ya Rais wa Tanzania na mfanyabiashara raia wa Zimbabwe Wicknell Chivayo bila kuzingatia mizania.
“Jamii Forums ilishindwa kutafuta maoni ya Mamlaka husika/Msemaji wa Rais/Serikali, kuthibitisha uhalisia wa picha (za Rais na Chivayo) zilizotumika, na hivyo kuuaminisha Umma taarifa za upande mmoja,” imesema taarifa ya Jamii Forums ikinukuu maamuzi ya TCRA.
Kwa hukumu hiyo Jamii Forums pamoja na majukwaa yake yote ya mtandaoni haitaweza kurusha taarifa za uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba 29, mwaka huu kama ambavyo imekuwa ikifanya miaka.ya nyuma kwa kuwa itakuwa ndani ya kipindi cha adhabu.
Hii si mara ya kwanza kwa TCRA kufungia chombo cha habari Tanzania.
Oktoba 2024 TCRA ilisitisha leseni zote za kuchapisha maudhui mtandaoni za kampuni ya Mwananchi Communication Ltd kwa kwa tuhuma za kuchapisha maudhui yaliyokiuka Sheria za nchi na kuleta tafsiri hasi kwa Taifa.
Latest
