Mahakama yaamuru kesi ya Lissu kutorushwa mubashara
- Yasema hatua hiyo italinda mashahidi raia wa kesi hiyo.
- Chombo cha habari, raia watakaokiuka amri hiyo kukiona.
Arusha. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Franco Kiswaga ameamuru kesi ya jinai namba 8607/2025 inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutorushwa mubashara hadi pale itakapotangazwa vinginevyo.
Uamuzi huo umetolewa kwa lengo la kuficha utambulisho wa mashahidi raia wa kesi hiyo iliyoanza kuunguruma Aprili 10, mwaka huu baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa Aprili 9 akiwa katika mkutano wa Chadema Mbinga, mkoani Ruvuma akikabiliwa na shtaka la uhaini.
Akizungumza baada ya kutajwa kwa Shauri hilo leo Agosti18, 2025 Hakimu Kiswaga amesema kurushwa mubashara kwa matangazo ya kesi hiyo kutafanya utambulisho wa mashahidi kufichuka baada ya kuifikia hadhira kubwa.
“Committal proceedings’ yote mahakama inaamuru isionyeshwe moja kwa moja kwa kuwa shahidi wanaopaswa kulindwa ikifanya hivyo hawatalindwa bali watajulikana kwa namna ambavyo kama amri ya makamu kuu ilivyoelekeza, hivyo inaamriwa hivyo,” amesema Kiswaga.
Kutokana na amri hiyo, mwenendo wa kesi inayomkabili Lissu hauruhusiwi kusambazwa moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii au aina nyingine nyingine ya uenezaji matangazo ya video wakati wa kesi ikiendelea ndani ya mahakama.
Hata hivyo, imebainishwa kuwa kesi hiyo itaendelea kuwa ya wazi yaani open court ikiwaruhusu waandishi wa habari, ndugu pamoja na wafutiliaji wengine kuhudhuria.
Kiswaga pia amesema kwa chombo chochote cha habari kinachotaka kurusha mubashara matangazo hayo kinahitaji kibali rasmi cha mahakama hiyo na uthibitisho wa kwamba watalinda mashahidi wa kesi hiyo na watakokiuka maagizo hayo watachukuliwa hatua.
“Amri nyingine kila mtu au chombo cha habari kitakachoenda kinyume na maelekezo ya Mahakama Kuu kwa kurusha kuchapisha au kusambaza nyaraka za ulinzi wa shaidi bila idhini ya mahakama hatua stahiki zitachukuliwa kwa kuwa ilikuwa ni amri halali ya Mahakama Kuu,” amesema Kiswaga.
Aidha, Mahakama hiyo imebainisha kuwa mshtakiwa atakuwa na nafasi kamili ya kusikia muhtasari wa taarifa na kuwasilisha maombi yoyote kuhusiana na haki ya kusikilizwa kwa usawa katika taratibu za kesi hiyo na hakuna ambacho kitazuia mshtakiwa au utetezi wake kuwasilisha maombi yanayofaa ili kuhakikisha kwamba haki inahifadhiwa.
Latest



