Tanzania ina vyama vingapi vya siasa?

August 12, 2025 3:41 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Oktoba 29, 2025 Tanzania inaenda kuandika historia nyingine kwa kufanya Uchaguzi Mkuu ambapo Watanzania watachangua wawakilishi wao yaani madiwani, wabunge na Rais.

Huo utakuwa Uchaguzi Mkuu wa saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mwaka 1992. 

Vyama 18, kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu, vimethibitisha kushiriki uchaguzi huo isipokuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema ambacho hakishiriki uchaguzi bila ya mabadiliko wanayoyataka kufanyika. 

Tathmini iliyofanywa na Nukta Habari imebaini kwa Watanzania wengi wanafahamu idadi ndogo ya vyama vya siasa hususan vile maarufu tu kama CCM, Chadema, CUF, ACT-Wazalendo, TLP, NCCR-Mageuzi na hivi sasa Chaumma.

Huenda umaarufu wa vyama hivyo unatokana na kushiriki kuunda Serikali, kuwa na viongozi maarufu, migogoro ya ndani ya vyama au kupokea wanachama mashuhuri kutoka vyama vingine.

Sasa  kama wewe ni miongoni mwa wasiofahamu vyama vya siasa vilivyopo nchini Tanzania makala hii ni kwa ajili yako. Hapa tunaangazia vyama vya  siasa 19 vilivyosajiliwa rasmi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hadi kufikia Machi 17, 2025. 

Chama Cha Mapinduzi CCM

Chama cha Mapinduzi (CCM), kilipata usajili wa kudumu Julai 1, 1992 kwa namba 0000001.

Ndicho chama tawala nchini na kimekuwa madarakani tangu kuundwa kwake mwaka 1977 kufuatia muungano wa Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) 

Mwenyekiti wake ni Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Tanzania, na Katibu Mkuu ni Dk Emmanuel Nchimbi.

The Civic United Front (CUF) 

The Civic United Front (CUF) au Chama cha Wananchi, kimesajiliwa rasmi Januari 21, 1993 kwa namba 0000002.

CUF ni miongoni mwa vyama vilivyokuwa na ushawishi mkubwa hasa visiwani Zanzibar kupitia siasa za upinzani. Mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahim Haruna Lipumba na Katibu Mkuu ni Husna Abdalla Mohammed.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilisajiliwa Januari 21, 1993 kwa namba 0000003.

Chadema inatambulika kama chama kikuu cha upinzani Tanzania na umaarufu wake unatokana na siasa za kiuanaharakati na viongozi wenye misimamo kama Tundu Lissu, ambaye ndiye Mwenyekiti wa chama, huku John Mnyika akiwa Kaimu Katibu Mkuu.

Chadema hawatashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kutokana na kutokukubaliana na baadhi ya taratibu za uendeshaji uchaguzi ambazo walitaka ziboreshwe.

Union for Multiparty Democracy (UMD)

Union for Multiparty Democracy (UMD), kilisajiliwa Januari 21, 1993 kwa namba 0000004, kinaongozwa na Mwenyekiti Mohamed Omari Shaame na Katibu Mkuu Moshi Rashid Kigundula.

NCCR-Mageuzi

National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), kilisajiliwa Januari 21, 1993 kwa namba ya usajili 0000005.

Chama Cha NCCR kimewahi kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za upinzani miaka ya 1990, kikihusishwa na viongozi waliowahi kuwa mashuhuri kama Augustino Mrema na James Mbatia.

Hivi sasa kinaongozwa na Kaimu Mwenyekiti Haji Ambari Khamis na Kaimu Katibu Mkuu Ameir Ali Mshindani.

National League for Democracy (NLD)

NLD nacho kilipata usajili wa kudumu Januari 21, 1993 kwa namba 0000006.

Kinaongozwa na Mwenyekiti Mfaume Khamis Hassan na Katibu Mkuu Doyo Hassan Doyo.

United Peoples’ Democratic Party (UPDP)

Chama hiki kilisajiliwa Februari 4, 1993 na kupewa namba ya usajili 0000008. Mwenyekiti wake ni Twalib Ibrahim Kadege na Katibu Mkuu Hamadi Mohamed Ibrahim.

NRA, TADEA na TLP

Vyama vingine vilivyopata usajili wa kudumu mwaka 1993 ni pamoja na National Reconstruction Alliance (NRA), kilichosajiliwa Februari 8, 1993 kwa namba 0000009, na kinaongozwa na Mwenyekiti Khamis Faki Mgau na Katibu Mkuu Hassan Kisabya Almas.

Chama Cha African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA), kilisajiliwa Aprili 5, 1993 kwa namba 00000011, kinaongozwa na Mwenyekiti Juma Ali Khatib. Picha l Full Shangwe

African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA), kilichosajiliwa Aprili 5, 1993 kwa namba 00000011, kinaongozwa na Mwenyekiti Juma Ali Khatib na Katibu Mkuu Saleh Msumari pamoja na Tanzania Labour Party (TLP), kilichosajiliwa Novemba 24, 1993 kwa namba 00000012.

Chama Cha TLP kiliwahi kujipatia umaarufu mwanzoni mwa mfumo wa vyama vingi kupitia kiongozi wake wa zamani, marehemu Augustino Mrema. 

Hivi sasa TLP inaongozwa na Mwenyekiti Richard Shadrack Lyimo na Katibu Mkuu Yustus Mbatina Rwamugira.

United Democratic Party (UDP)

United Democratic Party (UDP), kilisajiliwa Machi 24, 1994 kwa namba 00000013.

Chama hiki ndio kilifunga dimba kwa usajili wa vyama katika miaka ya tisini. UDP ndio chama chenye  Mwenyekiti aliyekaa madarakani muda mrefu zaidi, John Momose Cheyo, ambaye bado anakiongoza, huku Katibu Mkuu akiwa Saum Hussein Rashid.

Chama cha Demokrasia Makini (Makini)

Miaka ya 2000, Chama cha Demokrasia Makini (Makini), kikafungua dimba la usajili wa kudumu. Novemba 15, 2001 chama hiki kilipata usajili namba 00000053, kwa sasa kinaongozwa na Mwenyekiti Coaster Jimmy Kibonde na Katibu Mkuu Ameir Hassan Ameir.

Democratic Party (DP)

Mwaka mmoja baadae yaani Juni 7,  2002, Chama Cha Democratic Party (DP), Nacho kikapata usajili wa kudumu wenye namba 00000057.Kinaongozwa na Mwenyekiti Philipo John Fumbo na Katibu Mkuu Abdul Juma Mluya.

Sauti ya Umma (SAU)

Wakati Tanzania ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu mwaka 2005, chama kipya cha siasa kikaanzishwa na kupewa jina la Sauti ya Umma (SAU),.

Kilipata usajili wa kudumu  Februari 17, 2005 kwa namba 00000066, na kinaongozwa na Mwenyekiti Bertha Nkango Mpata na Katibu Mkuu Majalio Paul Kyara.

Alliance for African Farmers Party (AAFP)

Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Tanzania ikapta chama kingine cha Alliance for African Farmers Party (AAFP), kilichosajiliwa Novemba 3, 2009 kwa namba 00000067, chama hiko kinaongozwa na Mwenyekiti Said Soud Said na Katibu Mkuu Rashid Ligania Rai.

Chama cha Kijamii (CCK)

Chama cha Kijamii (CCK), kilisajiliwa Januari 27, 2012 kwa namba 00000079, kinaongozwa na Mwenyekiti David Daudi Mwaijojele na Katibu Mkuu Masoud Ali Abdallah.

Alliance for Democratic Change (ADC)

Mwaka huo huo wa 2012, Chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC), kilisajiliwa Agosti 28, 2012 kwa namba 00000080 na kinaongozwa na Mwenyekiti Shaban Haji Itutu na Katibu Mkuu Mwalimu Hamad Azizi.

Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma)

Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kilisajiliwa Juni 4, 2013 kwa namba 00000081.

Awali kimejipatia maarufu kutokana na sera ya Mwenyekiti wake Hashim Rungwe Spunda ambaye amekuwa akijinasibu iwapo chama hicho kitashinda uchaguzi miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele ni kugawa chakula cha ubwabwa kwa wananchi.

Chama hicho kimepata umaarufu wa hivi karibuni baada ya wafuasi waliaokuwa Chadema kujiunga na chama hicho baada ya kutokubaliana na msimamo wa kutoshiriki uchaguzi.

Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo)

ACT-Wazalendo, ndio chama cha mwisho kupata usajili wa kudumu nchini Tanzania Mei 5, 2014 kwa namba 00000083.

Licha ya upya wake ACT ni miongoni mwa vyama vikuu vya upinzani hasa visiwani Zanzibar, kikiongozwa na Kiongozi wa Chama Dorothy Jonas Semu, Mwenyekiti Othman Masoud Othman na Katibu Mkuu Ado Shaibu Ado.

Umaarufu wake umekuzwa na wanasiasa waliopata nafasi kubwa serikalini, akiwemo marehemu Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Benard Membe.

Vipi kwa upande wako ulikuwa unafahamu vyama vingapi vya siasa, tuambie kwenye maoni.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks