CCM kukusanya Sh100 bilioni kufanikisha kampeni Uchaguzi Mkuu 2025

August 11, 2025 6:03 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Itafanyika kesho Agosti 12, katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga  kufanya changisho (harambee) na kukusanya Sh100 bilioni zitakazotumika wakati wa kampeni ya kuwanadi wagombea wa chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema fedha hizo zitatumika kugharamia vifaa na huduma mbalimbali ikiwemo magari, mabango, vipeperushi, sare na gharama nyingine muhimu.

Kwa mujibu wa Nchimbi, tukio hilo lililoridhiwa na Kamati Kuu ya CCM litafanyika Agosti 12, 2025, katika ukumbi wa Mlimani City na kuongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Katika tukio hilo wanachama na wadau watapata fursa ya kutoa michango yao kupitia akaunti maalum za benki, na itaendelea kupokelewa hadi kipindi cha kampeni kitakapokaribia kumalizika.

Hata hivyo, Dk Nchimbi amesema CCM haitapokea michango itakayoathiri uhuru wa nchi au kuidhalilisha.

“Tutaainisha kujua michango hii inatoka wapi, Ile inayodhalilisha heshima au inapoteza uhuru wa Taifa letu, hatuwezi kuipokea,” amesema Dk Nchimbi.

Nchimbi ameongeza kuwa lengo la harambee ni kutoa nafasi kwa kila mwanachama na mpenzi wa chama kushiriki kuunga mkono juhudi za chama, licha ya CCM kuwa miongoni mwa vyama vyenye rasilimali nyingi nchini.

Aidha, pamoja na kuwa tukio hilo kufanyika kipindi ambacho mchakato wa kuteua wagombea wa ubunge bado haujakamilika, halitaathiri maamuzi ya mwisho yanayotarajiwa kufanyika karibuni.

“Hakuna mtu ataenda kuteuliwa eti kwa sababu kaja kwenye shughuli ile akachangia bilioni 20… hatuwezi kuitisha kikao cha maadili cha dharura kwa sababu wewe umetoa milioni 20,” amesema Nchimbi.

Itakumbukwa kuwa tayari mgombea wa nafasi ya Urais pamoja na mgombea mwenza kwa tiketi ya chama hicho tayari wameshachukua na kujaza fomu ambapo kwa sasa fomu hiyo inazungushwa katika mikoa yote nchini kutafuta wadhamini.

Vyama vingine vya siasa vinaendelea na michakato ya kuteua wagombea pamoja na kuchukua fomu katika ofisi za Tume huru ya Uchaguzi (INEC).

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks