Wawili kati ya 11 waliotimkia CCM kutoka Chadema watoboa kura za maoni 2025

August 6, 2025 11:16 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Jesca Kishoa na Kunti Majala pekee ndio walioweza kushinda kwenye majimbo waliyogombea.

Dar es Salaam. Mbivu na mbichi katika uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi zimeshajulikana mara baada ya wajumbe wa chama hicho kukamilisha kazi ya kuwapigia kura wawakilishi wa majimbo na kata kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.

Macho na masikio ya Watanzania wengi yalikuwa kwenye nafasi za ubunge ambako kulionekana kuwa na mchuano mkali ndani ya chama hicho.

Ushindani huo ulitokana na ongezeko la wanachama kutaka kuwania nafasi hiyo huku wengine wakitoka katika vyama vyao na kujiunga na CCM ili kutanua mawanda ya kupata nafasi ya uongozi ngazi ya jimbo.

Miongoni mwa waliojiunga na CCM ni pamoja na baadhi ya waliokuwa wabunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo 11 kati yao waliteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwenda kuomba kura kwa wajumbe.

Hata hivyo, Nukta Habari imebaini kuwa kati ya 11 ni wawili tu waliotoboa kwenye hatua ya kura za maoni, huku wengine wakishindwa kufua dafu mbele ya washindani wao waliopata kura nyingi zaidi.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura za maoni yaliyopatikana, Jesca Kishoa na Kunti Majala ndio walioshinda kwenye majimbo waliyogombea, na iwapo Kamati Kuu ya CCM haitafanya uamuzi tofauti, basi wawili hao ndio watakaobeba bendera ya chama hicho tawala katika uchaguzi wa wabunge katika majimbo husika.

Jesca Kishoa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema, ameibuka mshindi katika Jimbo la Iramba Mashariki, mkoani Singida kwa kupata kura 5,946 sawa na asilimia 56.8 ya kura zote 10,458 zilizopigwa. 

Kwa upande mwingine, Kunti Majala naye ameonyesha kuwa si wa kubezwa katika siasa za ndani ya chama. Ameshinda kura za maoni katika Jimbo la Chemba, Dodoma kwa kura 5,809, akiwashinda wapinzani wake watano.

Hata hivyo, hali haikuwa nzuri kwa waliobaki. Wanasiasa waliowahi kushika nafasi muhimu katika siasa za upinzani, kama Ester Bulaya, Esther Matiko, na Cecilia Paresso, wamejikuta hawajaaminika vya kutosha mbele ya wanachama wa CCM kwenye kura hizo za ndani.

Bulaya, aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunda Mjini kwa tiketi ya Chadema, ameshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 625 pekee, akiachwa mbali na mshindi Robert Maboto aliyepata 2,545 na Kambarage Wasira aliyepata 2,032.

Esther Matiko, aliyekuwa mbunge wa Tarime Mjini, naye amemaliza wa tatu kwa kura 196, nyuma ya Michael Kembaki aliyepata 1,568. 

Katika Jimbo la Karatu, Cecilia Paresso amemaliza nafasi ya pili kwa kura 1,341, akiachwa mbali na, Daniel Awack, aliyeshinda kwa kura 7,884.

Wengine waliokwamia katika kura hizo za maoni ni pamoja na Hawa Mwaifunga, jimbo la Tabora Mjini, aliyepata kura 326 dhidi ya mshindi Shaaban Mrutu aliyepata 6,612, pamoja na Nusrati Hanje, Grace Tendega, Felister Njau, Sophia Mwakagenda, na Stella Fiyao.

Awali, wabunge hao 11 walikuwa miongoni mwa kundi la wabunge 19 wa Viti Maalum waliofukuzwa Chadema mwaka 2020, kisha baadaye kutangaza kujiunga na CCM. 

Kwa sasa macho na masikio yameelekezwa kwenye Kamati Kuu ya CCM ambayo itatoa uamuzi wa mwisho juu ya majina yatakayopitishwa kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks