Dk Biteko: Waandishi wa habari zingatieni maadili
- Awahasa watanzania kuwa wamoja bila kuzingatia tofauti za kisiasa
- Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imesajili waandishi 2,900 kupitia Mfumo wa Kidijitali wa TAI Habari.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao ili kudumisha amani na usalama wa taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuripoti kwa usawa, na kushiriki kikamilifu kukabiliana na habari potofu.
Dk Biteko aliyekuwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau kujadili mchango wa sekta ya habari katika kufanikisha uchaguzi mkuu 2025, amesisitiza kuwa kipindi cha uchaguzi kinakumbwa na mitazamo tofauti ya kisiasa, hivyo wanahabari wana jukumu la kuelekeza taifa kwa kutumia kalamu zao kwa haki na busara.
“Pamoja na kwamba tutatofautiana mawazo na mitazamo, tusalie na jambo moja kuwa sisi ni Watanzania wenye nia ya kujenga amani ya nchi yetu,” amesema Dk. Biteko.

Dk. Biteko ameongeza kuwa waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kuchambua na kuchuja taarifa kabla ya kuwafikia wananchi, jambo linalowapa mamlaka ya kuathiri namna jamii inavyoelewa sera na mipango ya viongozi wa kisiasa.
“Unaweza ukaongea mambo mengi lakini mwandishi wa habari ndiye anaamua walaji awapelekee nini,” ameongeza Dk. Biteko.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali hadi sasa Tanzania ina jumla ya vyombo vya habari 1,117. Miongoni mwao ni magazeti 375, vituo vya redio 247, televisheni 68, vyombo vya habari mtandaoni 355, na blogu 72.
Aidha utafiti wa mwaka 2022 uliofanywa na Afro Barometer na Repoa unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 76 ya Watanzania hupata taarifa za kisiasa kupitia redio na televisheni.
Sekta ya habari ni mhimili wa uchaguzi huru na haki
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema mkutano huo umefanyika ili kutambua mchango wa vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Vyombo vya habari ni mhimili muhimu sana katika maendeleo ya taifa letu,” amesisitiza Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi amebainisha kuwa katika mazingira ya sasa yenye changamoto ya taarifa potofu, lugha za chuki na udhalilishaji unaotokana na matumizi hasi ya mitandao ya kijamii, ni muhimu waandishi wawe na uwezo wa kuchuja na kutoa taarifa zilizo sahihi na zenye kuleta uelewa sahihi kwa wananchi.
Waandishi 2,900 wasajiliwa mfumo wa kidijitali
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi ameeleza kuwa hadi sasa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imesajili waandishi 2,900 kupitia Mfumo wa Kidijitali wa TAI Habari, unaorahisisha uchakataji wa taarifa za mwandishi na kumpatia kitambulisho cha kidijitali (Digital Press Card).
Kabudi amesema hatua hiyo inalenga kuongeza uwajibikaji, uaminifu na kurahisisha utambuzi wa waandishi wenye sifa halali, hasa kuelekea msimu wa uchaguzi ambapo taaluma ya uandishi inakuwa na jukumu kubwa la kuelimisha jamii.
Latest



