INEC yaongeza majimbo Tanzania, Bunge likifikia wabunge zaidi 400

May 12, 2025 5:01 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Majimbo mapya yanajumuisha Kivule, Uyole na Chamazi.
  • Uamuzi huo utakaongeza wabunge wanane na kufanya bunge liwe na wabunge wasiopungua 401. 

Dar es Salaam.Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeongeza majimbo mapya manane ya uchaguzi nchini, uamuzi utakaongeza ukubwa wa Bunge na kulifanya liwe na wabunge zaidi ya 400 baada ya Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba mwaka huu.

Katika mkutano wake na wanahabari jijini Dodoma, leo Mei 12, 2025, Mwenyekiti wa INEC Jaji Jacobs Mwambegele amesema hatua hiyo imefikiwa kwa mujibu wa sheria baada ya kukaa na wadau wa baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa na kujiridhisha na taarifa za maombi zilizowasilishwa tume.

Kuongezeka kwa majimbo 8 ya uchaguzi kunafanya kufikia jumla ya majimbo 272 ya uchaguzi kutokea majimbo 264 yaliyo kuwepo wakati wa uchaguzi mwaka 2020. Picha | INEC

Majimbo nane yaliyoongezwa yanajumuisha mawili yaliyopo Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni Jimbo la Kivule lililogawanywa kutoka Jimbo la Ukonga, na jimbo la Chamazi lililogawanywa kutoka Jimbo la Mbagala.

Kwa mkoa wa Dodoma limeanzishwa Jimbo jipya la Mtumba lililogawanywa kutoka jimbo la Dodoma Mjini na Jimbo jipya la Uyole lililogawanywa kutoka Jimbo la Mbeya Mjini kwa mkoa wa Mbeya.

Majimbo mengine ni Jimbo la Bariadi Mjini kwa mkoa wa Simiyu, Jimbo la Katoro na Chato Kusini mkoani Geita, pamoja na Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga.

Hatua hiyo ya INEC inatarajiwa kuongeza idadi ya wabunge wanane bungeni katika Bunge la 13 na kufanya idadi ya wabunge wasiopungua 401 kutoka 393 waliopo sasa.

Idadi hiyo itajumuisha wabunge 272 watakao gombea kutoka katika majimbo yao, wabunge wa viti maalum, wabunge 10 watakao teuliwa na Rais, na wawakilishi watano kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kuongezeka kwa majimbo 8 ya uchaguzi kunafanya kufikia jumla ya majimbo 272 ya uchaguzi kutokea majimbo 264 yaliyo kuwepo wakati wa uchaguzi mwaka 2020 ambapo kati ya majimbo 272 majimbo 222 yapo Tanzania Bara na majimbo 50 kutoka Zanzibar. 

Jaji Mwambegele amesema kuwa ukiachilia mbali ongezeko la idadi ya majimbo ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria, INEC imezingatia vigezo vingine ikiwemo idadi ya wabunge wanawake wa viti maalum pamoja na uwezo wa ukumbi wa Bunge kwa kuzingatia idadi ya wabunge ambayo Bunge linaweza kubeba. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume ili eneo fulani liweze kukidhi kuwa Jimbo la uchaguzi linatakiwa kuwa na idadi ya watu 600,000 kwa majimbo ya mjini na watu 400,000 kwa majimbo ya maeneo ya vijijini.

Pamoja na ongezeko la Majimbo ya Uchaguzi, tume hiyo pia imeongeza kata tano kwa upande wa chaguzi za madiwani na kufanya kufikia jumla ya kata 3,960 kutoka kata 3,955 zilizoshiriki uchaguzi mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Idadi ya Watu katika Majimbo ya Uchaguzi Tanzania, iliyotolewa Disemba 2022, mkoa wenye majimbo mengi ni Mkoa wa Mjini Magharibi wenye majimbo 19 ukifuatiwa na mikoa ya Tabora na Tanga yenye majimbo 12 kila mkoa huku mikoa yenye majimbo machache ikiwa ni Kusini Unguja, Katavi na Rukwa yenye majimbo matano kila mkoa.

Je, kuongezeka kwa idadi ya wabunge bungeni ni kiashiria cha kuongezeka kwa chachu ya maendeleo na uwajibikaji?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks