Wizara ya Elimu yaomba bajeti ya zaidi Sh2.4 trilioni 2025/26

May 12, 2025 4:13 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Kamati ya Bunge yaonya juu ya Serikali kutotoa fedha zilizoidhinishwa.
  • Yasema inaathiri utekelezaji wa baadhi ya shughuli za wizara.

Dar es Salaam. Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh2.436 trilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2025/26, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh471.1 bilioni ndani ya mwaka mmoja ikichagizwa zaidi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ongezeko la mikopo ya elimu ya juu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda emelieleza Bunge leo Mei 12, 2025 jijini Dodoma kuwa mapendekezo hayo ya bajeti ni sawa ongezeko la asilimia 24 kutoka Sh1.965 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025. 

Serikali imepanga kutumia bajeti hiyo katika majukumu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kampasi 16 za taasisi za elimu ya juu ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi na ununuzi wa vifaa saidizi kama vitimwendo, kompyuta, vishikwambi na vinasa sauti vya kidigiti.

Viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa Bungeni jijini Dodoma, wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo. Picha/ Wizara ya Elimu/X.

Prof. Mkenda amesema kati ya fedha hizo zinazoombwa, matumizi ya kawaida ni Sh688.61 bilioni sawa na asilimia 28.26 ya bajeti yote yanayojumuisha mishahara ya watumishi wa umma chini ya wizara hiyo ya Sh635.25 bilioni. Matumizi mengine ya kawaida ni Sh53.36 bilioni. 

Sehemu kubwa ya bajeti hiyo Sh1.75 trilioni au theluthi mbili ya bajeti hiyo inatarajiwa kugharamia miradi ya maendeleo.

Prof. Mkenda amesema bajeti hiyo pia itaendelea kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kuhakikisha inanufaisha idadi kubwa zaidi. 

“Serikali itaendelea kutoa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wenye sifa ili kuongeza fursa za elimu ya juu nchini, itaongeza idadi ya wanafunzi wanufaika wa elimu ya juu kutoka 245,314 mwaka 2024/2025 hadi wanafunzi 252,773 kwa mwaka 2025/2026,” amesema Prof Mkenda. Idadi hiyo ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 177,925 waliorekodiwa mwaka 2021/2022.

Serikali, imesema itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 10,000 kwa ngazi ya stashahada wa fani za kipaumbele.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiwasilisha hotuba ya bajeti Bungeni Jijini Dodoma. Picha/ Wizara ya Elimu/X.

Kumekuwa na presha kubwa kwa Serikali kuongeza na kutekeleza ipasavyo bajeti za mikopo ya elimu ya juu ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wakiwemo wanaosoma ngazi ya stashahada wananufaika nayo.

Prof Mkenda ameeleza kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh570 bilioni mwaka 2021/2022 hadi Sh787.4 bilioni mwaka 2024/2025. 

Kati ya fedha zilitengwa fedha za ndani ni Sh1.19 trilioni na fedha za nje Sh560.83 bilioni.

Licha ya kuongeza bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeeleza kuwa mwenendo wa ukusanyaji mapato hauendani na kasi ya jumla ya ongezeko la bajeti. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amesema ongezeko la bajeti ya matumizi kwa asilimia 24 haliendani na kasi ya ongezeko la mapato la asilimia 6.4, jambo linaloweza kuathiri utekelezaji wa shughuli za wizara.

Makadirio ya mapato kati ya wizara na taasisi zake yameongezeka kwa asilimia tofauti wakati wizara ina ongezeko la asilimia 13.4, taasisi zinaongezeko la asilimia 3.7… ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2024/2025 ulionyesha ugumu wa kufikia lengo,” amesema Sekiboko. 

Utegemezi katika miradi ya maendeleo unatarajiwa kuongezeka katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 2025

Utegemezi wa fedha za nje kwa miradi ya maendeleo unatarajiwa kuwa asilimia 32 mwaka 2025/26 kutoka asilimia 22.2 katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Sanjari na maoni hayo kamati hiyo pia imebainisha kutotolewa kwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa wakati kunaweza kuathiri utendaji baadhi wa shughuli za wizara.

Katika mwaka wa fedha ujao, wizara hiyo imepanga kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria, uandaaji wa miongozo na utoaji wa mafunzo na kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali. 

Vipaumbele vingine vya wizara hiyo ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu pamoja na kuongeza na kuimarisha ubora elimu ya juu 

Vile vile, kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks