Tanzania, Msumbiji zasaini makubaliano kufungua fursa kibiashara

May 8, 2025 5:38 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni mwa makubaliano ni kubadilishana wafungwa baina ya nchi hizo.

Dar es Salaam. Serikali za Tanzania na Msumbiji zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika maeneo sita yakiwemo kubadilishana wafungwa na uanzishwaji wa kituo cha pamoja cha forodha mpakani ili kuchochea shughuli za biashara na uchumi baina ya nchi hizo majirani. 

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Mei 7, 2025, katika Ikulu ya Dar es Salaam kufuatia ziara ya kiserikali ya siku tatu ya Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, ambaye yuko nchini kwa mwaliko rasmi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Nchi hizo zimekubaliana kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kufanya biashara kwa urahisi zaidi hasa katika maeneo ya mpakani. Picha | Ikulu Tanzania.

Rais Samia amewaeleza wanahabari baada ya mazungumzo na mgeni wake kuwa licha ya uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji, bado kuna pengo katika ushirikiano wa kiuchumi ambalo linapaswa kufanyiwa kazi kwa pamoja.

“Ushirikiano wetu wa kiuchumi bado haujaenda sambamba na uhusiano wetu wa kisiasa na kidiplomasia,” amesema Rais Samia.

Hati za makubaliano zilizosainiwa leo baina ya nchi hizo zinahusisha uanzishwaji wa kituo cha pamoja cha forodha, mkataba wa kubadilishana wafungwa, mkataba wa kubadilishana wanafunzi, ushirikiano katika masuala ya utamaduni, ushirikiano baina ya mamlaka za dawa na vifaa tiba pamoja na ushirikiano baina ya mashirika ya habari. 

Rais Samia amesema kuwa nchi hizo zimekubaliana kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kufanya biashara kwa urahisi zaidi hasa katika maeneo ya mpakani.

Tanzania na Msumbiji, amesema, zitashirikiana kuanzisha vituo vya pamoja vya biashara mpakani ili kurahisisha shughuli za kiuchumi, pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara, anga na baharini kwa usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Majadiliano yao yaligusia pia umuhimu wa kushirikiana katika masuala ya nishati, hasa gesi asilia, pamoja na kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi, utalii na madini.

“Maeneo mengine ya ushirikiano ambayo tumekubaliana kuendeleza uhusiano ni kwenye sekta za mawasiliano, madini, elimu na afya,” ameongeza Rais Samia.

Rais Chapo, anayehitimisha ziara yake kesho, amesema kuwa Msumbiji iko tayari kushirikiana kwa karibu zaidi na Tanzania ili kuendeleza mafanikio ya pamoja akisisitiza kuwa historia ya ukombozi inayounganisha mataifa haya mawili iwe chachu ya maendeleo ya sasa.

Rais Chapo, anayehitimisha ziara yake kesho, amesema kuwa Msumbiji iko tayari kushirikiana kwa karibu zaidi na Tanzania ili kuendeleza mafanikio ya pamoja, Picha | Ikulu Tanzania.

Rais Chapo pia anatarajiwa kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika na mradi wa reli ya kisasa (SGR), kabla ya kuelekea Zanzibar kwa ziara ya siku moja.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikuza bidhaa kama vinywaji, saruji, tumbaku na mafuta, huku ikiagiza mbao, bidhaa za alumini na sukari kutoka Msumbiji. Hata hivyo, mwenendo wa biashara baina ya nchi hizo mbili umeduma baada ya takwimu za Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tantrade) kubainisha kuwa thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nchini Msumbiji kupungua kidogo kutoka Dola za Marekani 15.8 milioni mwaka 2017 na Dola za Marekani 15.4 milioni kufikia 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks