Wizara ya Katiba na Sheria yaomba Sh687 bilioni kutekeleza vipaumbele 22

April 30, 2025 5:43 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Nchini na kubainisha na kutatua migogoro ya kisheria kwa wananchi na wadau wengine.

Dar es salaam. Wizara ya Katiba na Sheria imeliomba Bunge liidhinishe bajetii ya Sh687.6 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele 22 ikiwemo utoaji wa huduma za kisheria na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kote nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, aliyekuwa akiwasilisha maombi hayo bungeni leo Aprili 30, 2025 amesema  bajeti hiyo inajumuisha fedha kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengineyo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ndani na nje ya nchi.

“Kati ya fedha zinazoombwa, Sh135.9 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, Sh389.4 bilioni kwa matumizi mengine na Sh162.2 bilioni kwa miradi ya maendeleo,”amesema Dk Ndumbaro. 

Bajeti inayoombwa imeongezeka kwa Sh246.4 bilioni kulinganisha na mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 55.9 ambapo wizara iliidhinishiwa jumla ya Sh441.2 bilioni. Picha | Bunge la Tanzania.

Kwa mujibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, bajeti hiyo inaenda kutekeleza vipaumbele kama kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa watu wenye uhitaji pamoja na kushughulikia masuala ya kikatiba pamoja na kutoa elimu ya katiba na uraia kwa umma.

Vipaumbele vingine ni kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Nchini, kubainisha na kutatua migogoro ya kisheria kwa wananchi na wadau wengine, kuimarisha mifumo ya utoaji haki ili haki ipatikane kwa wote na kwa wakati pamoja na kuboresha mfumo wa kitaifa na kuzingatia mifumo ya kikanda na kimataifa kuhusu haki za binadamu na utawala bora.

“Kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika masuala ya haki jinai na haki madai, kuwezesha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sekta ya sheria nchini, kuimarisha mifumo kisheria na kitaasisi katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kuimarisha usimamizi wa mikataba ya utajiri asili na maliasili za nchi ambazo wizara, idara na taasisi za Serikali zimeingia na wawekezaji,” inabainisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Aidha, Wizara ya Katiba na Sheria imesema itaendelea kuitaimarisha usimamizi, ufuatiliaji na majadiliano ya mikataba, kuimarisha mfumo wa uandishi, ufasiri na urekebu wa sheria, kuongeza uelewa kwa watendaji wa Serikali na wananchi kuhusu Sheria za Nchi pamoja na kuimarisha utafiti, tathmini na mapitio ya sheria kama sehemu ya vipaumbele vyake 22.

Vipaumbele vingine vitakavyotekelezwa Ili kuimarisha upatikanaji wa haki ni pamoja na kuendesha mashtaka ya jinai na kuimarisha shughuli za utenganishaji wa mashtaka na upelelezi; kuimarisha uratibu, usimamizi na uwakilishi katika kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika sekta ya sheria.

Waziri Ndumbaro amesema kuwa kwa ujumla ongezeko hilo limelenga kuboresha upatikanaji wa haki, kuimarisha miundombinu ya mahakama na taasisi nyingine za sheria pamoja na kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma za kisheria. Picha | Habari Leo.

“Kusimamia na kuendeleza elimu na taaluma ya sheria nchini, kuwezesha usajili wa matukio muhimu ya binadamu na kusimamia masuala ya ufilisi na udhamini, kuwezesha ajira, uteuzi, kuimarisha nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama. Kuimarisha mifumo ya Tehama kwa ajili ya kuboresha huduma za kisheria nchini na kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya sheria,” imeeleza Wizara ya Katiba na Sheria.

Hata hivyo, bajeti inayoombwa imeongezeka kwa Sh246.4 bilioni kulinganisha na mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 55.9 ambapo wizara iliidhinishiwa jumla ya Sh441.2 bilioni.

Uchambuzi uliofanywa na Nukta umebaini bajeti kwa ajili ya mishahara ya watumishi imeongezeka kwa asilimia 20 kutoka Sh112.4 bilioni mwaka 2024/25  hadi Sh135.9 bilioni mwaka huu.

Aidha, bajeti kwa ajili ya matumizi mengineyo imeongezeka kutoka Sh223.1 bilioni hadi Sh389.4 bilioni, sawa na ongezeko la  asilimia 74.5.

Bajeti ya miradi ya maendeleo nayo  imeongezeka kutoka Sh105.6 bilioni hadi Sh162.2 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 53.5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks