Jinsi ya kupunguza matumizi ya intaneti kwenye simu yako
- Ni kwa kutumia njia rahisi kupitia mipangilio ya simu yako (Settings).
Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu ambao wanatumia simu janja kuwasiliana na watu na kutafuta vitu mtandaoni kwa kutumia intaneti. Umekuwa ukijiuliza kwa nini unatumia kiwango kikubwa cha intaneti na inaisha kwa muda mfupi?
Siyo wewe peke yako unayepata changamoto hiyo. Watumiaji wengi wa intaneti katika simu zao kwa kujua au kutojua wamekuwa wakifanya makosa ambayo yanachangia bando za intaneti kuisha kwa haraka na kuwaongezea gharama ambazo haziko katika mipango yao.
Usihofu kwa sababu suluhu imepatikana. Baada ya kusoma mbinu nilizoeleza hapo chini, huenda ukapunguza matumizi ya intaneti katika simu yako na ukaendelea kufurahia ulimwengu wa kidijitali.
Tumia ‘Data Saver’ kwenye simu
Simu janja zina kipengele cha kidhibiti data (Data Saver) ambacho husaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya intaneti kwa kuzuia programu tumishi (apps) kutotumia intaneti bila ruhusa yako. Kwa kutumia mpangilio ya simu yako (Settings) unaweza kuzuia matumizi ya inteneti kwenye simu yako kwa kufuata hatua chache.

Kwa watumiaji wa simu za Android, nenda kwenye ‘Settings’ kisha chagua ‘Network & Internet’ gusa ‘Data Saver’ kisha washa. Kwa watumiaji wa simu za iPhone, nenda kwenye ‘Settings’ kisha chagua ‘Mobile Data’ washa sehemu iliyoiandikwa ‘Low Data Mode’
Hii itazuia apps ambazo hutumii kwa wakati huo kutokutumia intaneti mpaka pale utakapozifungua.
Tumia Wi-Fi pale inapohitajika
Moja ya njia bora za kupunguza matumizi ya intaneti ni kuhakikisha unatumia intaneti ya umma (Wi-Fi) badala ya simu yakoi. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na jukwaa la takwimu la Statista, watumiaji wengi wa simu huokoa hadi asilimia 60 ya intaneti wanapotumia Wi-Fi nyumbani au kazini. Hakikisha umewasha Wi-Fi auto-connect kwa maeneo unayoyafahamu kama nyumbani au ofisini. Hii itasaidia bando la intaneti ya simu yako isiishe mapema.

Punguza ubora wa video unazotazama
Video ni moja ya maudhui yanayotumia intaneti kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na picha au maandishi. Kulingana na taarifa iliyotolewa na kampuni inayotoa huduma za kulinganisha bei za huduma za simu na mtandao ya WhistleOut ya mwaka 2025, video za YouTube zenye ubora wa 1080p hutumia takribani 3GB kwa saa, wakati 480p hutumia karibu 500MB kwa saa.
Ili kupunguza ubora wa video unazotazama kwenye simu yako, fungua app ya YouTube nenda kwenye ‘Settings’ kisha chagua ‘Video quality preferences’ weka chaguo la ‘Data Saver Mode’

Kwa watazamaji wa video katika mtandao wa Netflix, unaweza kupunguza ubora wa video kwa kufungua ‘Netflix app’ kisha nenda kwenye ‘App Settings’ chagua ‘Cellular Data Usage’ kisha bofya ‘Save Data’
Zuia baadhi ya programu tumishi
Baadhi ya apps za simu yako huwa zinaendelea kutumia intaneti hata kama huzitumii. Kwa mujibu wa Google Support, apps kama Facebook, Instagram, na WhatsApp hutumia intaneti kupokea taarifa na kusasisha maudhui hata kama hujazifungua au kuzitumia wakati huo. Hii inaweza kufanya simu yako kupoteza kiasi kikubwa cha intaneti hata kama hutumii kwa wakati huo.
Ili kuzuia apps hizo kupitia mipangilio ya simu yako. Kwa watumiaji wa simu za Android nenda kwenye ‘Settings’ chagua ‘Apps & Notifications’ kisha bofya app unayoitaka baada ya hapo chagua ‘Mobile Data & Wi-Fi’ kisha zima chaguo la ‘Background Data’

Kwa watumiaji wa simu za iPhone nenda kwenye ‘Settings’ chagua ‘General’ kisha ingia mahali palipoandikwa ‘Background App Refresh’ zima kwa apps zisizo muhimu. Hii itahakikisha apps hazitumii intaneti wakati huzitumii moja kwa moja.
Tumia programu tumishi za Lite
Apps maarufu kama Facebook, X zamani Twitter, na Messenger zina matoleo ya Lite, ambayo hutumia intaneti kidogo kuliko apps za kawaida.

Kwa mujibu wa mtandao wa mauzo wa Android Authority, Facebook Lite hutumia chini ya asilimia 50 ya intaneti ukilinganisha na app ya kawaida ya Facebook. Unapopakua apps hizi kwenye Google Play Store au App Store, tafuta neno Lite ili kupata matoleo hayo. Matumizi ya App za Lite yanasaidia kupunguza matumizi ya intaneti kwenye simu yako.
Zuia upakuaji wa moja kwa moja wa maudhui
Kupokea au kupakua video na picha moja kwa moja kwenye apps za WhatsApp na Telegram huchangia inteneti kuisha haraka. Unaweza kuzuia hili lisitokee kwa kuboresha mpangilio wa simu yako.
Nenda kwenye ‘Settings’ ya WhatsApp, chagua ‘Storage and Data’ kisha nenda sehemu ya ‘Media Auto-Download’ weka chaguo la ‘Wi-Fi Only’

Kwa upande wa Telegram nenda kwenye ‘Settings’ chagua ‘Data and Storage’ kisha zima chaguo la ‘Auto-Download Media’ kwa inteneti ya simu. Hii itakusaidia kuzuia matumizi yasiyo ya lazima ya inteneti kwa kupakua mafaili kwa intentei ya umma pekee.
Tumia programu zinazopunguza matumizi ya intaneti
Baadhi ya programu zina teknolojia ya kuminya intaneti (Data Compression) ambayo husaidia kupunguza matumizi unapovinjari mtandaoni. Kwa mfano unaweza kupunguza matumizi ya intaneti kwenye Google Chrome kwa kuwasha ‘Lite Mode’ kwenye Settings. Pia Opera Mini nayo hutumia kiwango kidogo cha intaneti, ambapo TechRadar imeeleza kuwa inaokoa intaneti hadi asilimia 50.
Kwa kufuata mbinu hizi, unaweza kufurahia matumizi ya simu yako bila kuhofia gharama kubwa za intaneti.
Latest



