Nini hufanyika mara baada ya Papa kufariki?

April 22, 2025 12:37 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuteketeza Pete inayotumika kama mhuri ya kiongozi huyo
  • Uchaguzi wa Papa mpya hufanywa mara baada ya siku tisa za maombolezo na mazishi.

Dar es salaam. Kwa sasa, ulimwengu unaomboleza kifo cha aliyekuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Fransisko ambaye amefariki dunia Aprili 21, 2025. 

Mamilioni ya waamini na watu wa imani tofauti wanajiunga katika maombi na maombolezo, wakitafakari maisha ya huduma na upendo aliyoyaishi.

Lakini katika wakati huu wa huzuni, swali kubwa linabaki akilini mwa wengi. Je, nini hasa hutokea pale ambapo Papa anafariki dunia? Je, ni nani anayechukua usukani? Taratibu zipi hufuatwa? Na je, ni kwa namna gani Kanisa linaendelea mbele bila kiongozi wake wa juu kabisa?

Nukta Habari tunakuletea mfululizo wa taratibu za kihistoria, za kiimani na za kipekee ambazo zimekuwa zikifuatwa kwa karne nyingi mara baada ya kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki kufariki dunia. 

Kutangazwa kwa kifo cha Papa

Camerlengo ambaye ndiye kiongozi mwenye cheo cha juu ndani ya kanisa katoliki huthibitisha kifo cha Papa ambapo kitamaduni Papa huitwa jina lake la ubatizo mara tatu na kisha asipoitika kifo chake huthibitika. Baada ya hapo, Camerlengo huchukua pete ya Papa inayojulikana kama ‘Ring of the Fisherman’ na kuivunja ili kuzuia matumizi yoyote ya mihuri au mamlaka ya ofisi ya Papa aliyefariki.

Baada ya uthibitisho wa Camerlengo, Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican hutoa taarifa rasmi kwa dunia nzima baada ya tangazo hili bendera ya Vatican hupeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya maombolezo.

Camerlengo anahusika na mambo ya kiutawala na kifedha ya Vatican wakati wa kipindi cha mpito yaani baada ya kifo au kujiuzulu. Picha | Vatican News.

Camerlengo (kwa Kiitaliano) au ‘Chamberlain of the Holy Church’ ni cheo cha juu ndani ya Kanisa Katoliki, hasa katika Serikali ya Vatikani. Huyu ni kiongozi anayehusika na mambo ya kiutawala na kifedha ya Vatican wakati wa kipindi cha mpito yaani baada ya kifo au kujiuzulu kwa Papa na kabla ya kuchaguliwa Papa mpya.

Camerlengo hana mamlaka ya kiroho kama vile kutoa sakramenti juu ya Kanisa lote, bali anahusika na masuala ya utawala. Ni msimamizi mkuu wa Serikali ya Vatikani wakati hakuna Papa. Camerlengo anaweza kuwa Kardinali, na anateuliwa na Papa mwenyewe.

Siku tisa za maombolezo (Novemdiales)

Baada ya kifo cha Papa, Kanisa Katoliki huingia kwenye kipindi cha siku tisa za maombolezo kilichopewa jina la ‘Novemdiales’. Kila siku, Misa maalum hufanyika mjini Vatican kwa ajili ya kumuombea Baba Mtakatifu aliyeaga dunia.

Katika wakati huu, viongozi wa Kanisa kutoka kila kona ya dunia huanza kusafiri kwenda Vatican kwa ajili ya mazishi na maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya.

Mazishi ya Papa

Kwa kawaida, mwili wa Papa huwekwa kwenye majeneza matatu tofauti la kwanza likiwa ni jeneza la ndani la mbao laini, ambalo huwekwa hati maalum kuhusu maisha ya Papa, pamoja na medali mbalimbali za Kipapa. 

Baada ya kufungwa, jeneza hilo huwekwa ndani ya jeneza la pili la risasi linalolinda mwili  kuoza haraka na ikiwa ni ishara ya uzito wa heshima kwa Papa. 

Hatimaye, jeneza hilo huwekwa kwenye jeneza la tatu la mbao ngumu, ambalo linafungwa kwa misumari na mihuri rasmi kabla ya kuzikwa katika mapango ya chini ya Basilika ya Mtakatifu Petro.

Kabla ya kuzikwa mwili wake huwekwa wazi kwa waumini kutoa heshima zao za mwisho katika Basilika ya Mtakatifu Petro.

Hata hivyo, kwa kuzingatia maelekezo yake mwenyewe, mazishi ya Papa Fransisko yatafanyika tofauti na mapapa 91 waliomtangulia.

Mabadiliko katika mazishi ya Papa yalilenga kuonesha maziko ya Papa kuwa ni ya Mchungaji na Mfuasi wa Kristo na si ya mtu maarufu sana duniani. Picha | Vatican News

Papa Fransisko atazikwa katika jeneza moja la mbao badala ya majeneza matatu ya kifahari. Na mwili wake utazikwa katika Basilika ya Santa Maria Maggiore, mahali alipopendelea yeye mwenyewe.

Aidha, Vatican imefanya marekebisho makubwa namna ya kumzika Papa kutoka majeneza matatu hadi mawili na kuuaga mwili wa papa ukiwa ndani ya jeneza kutoka kuuga ukiwa wazi juu ya ubao hapo awali.

Marekebisho hayo yalisainiwa na Papa Fransisko Aprili 2024 ambapo kimsingi yalipitishwa awali na Papa Yohane Paulo II. Mabadiliko haya yalilenga kuonesha maziko ya Papa kuwa ni ya Mchungaji na Mfuasi wa Kristo na si ya mtu maarufu sana duniani. 

Sede Vacante 

Mara baada ya maziko ya Papa kufanyika huanza kipindi ambacho hujulikana kama ‘Sede Vacante’ ikimaanisha kuwa kiti cha Papa kiko wazi. Hiki ni kipindi ambacho shughuli zote kuu za Kanisa husimamiwa na Camerlengo hadi Papa mpya atakapochaguliwa. Katika kipindi hiki, hakuna maamuzi makubwa yanayofanywa, na maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya huanza.

Uchaguzi wa Papa mpya

Baada ya siku tisa za maombolezo na maziko ya Papa, makardinali wote wa Kanisa Katoliki wenye chini ya miaka 80 hukutana mjini Vatican kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya, unaoitwa Conclave

Neno hilo linatokana na Kilatini cum clave linalomaanisha “wakiwa ndani ya kufuli,” kwani makardinali hukaa mahali pa siri bila mawasiliano ya nje hadi watakapomchagua Papa mpya.

Conclave hufanyika ndani ya chumba kinachojulikana kama Sistine Chapel. Kura hufanyika kwa siri, na hakuna mtazamaji wala mawasiliano ya nje. 

Moshi mweusi huashiria Papa bado hajapatikana na mweupe huashiria Papa mpya amepatikana. Picha | USA Today.

Ili Kadinali aliyependekezwa achaguliwe kuwa Papa, ni lazima apate kura zisizopungua theluthi mbili ya kura zote. Katika kipindi chote za zoezi la kumpata Papa mpya kura huendelea hadi atakapopatikanaa. 

Na baada ya kila zoezi la upigaji kura, moshi hutolewa juu ya Sistine Chapel, moshi mweusi huashiria Papa bado hajapatikana na mweupe huashiria Papa mpya amepatikana.

Mara tu Papa mpya anapochaguliwa, hutoa jibu la kukubali kushika nyadhifa hiyo, na kuchagua jina atakalolitumia kama Papa.

Baadaye, Msemaji wa Conclave hutokea katika balkoni ya Basilika ya Mtakatifu Petro na kutangaza kwa kusema “Habemus Papam” yaani “Tunaye Papa”. Muda huu kengele kupigwa katika makanisa katoliki kote ulimwenguni kuashiria kuwa Papa mpya amepatikana.

Papa mpya hujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza na kutoa baraka yake kwa mji wa Roma na ulimwengu mzima ambapo baraka hiyo ya kwanza hujulikana kama ‘Urbi et Orbi’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks