Jeshi la magereza lakanusha kutoa taarifa ya alipo Tundu Lissu
- Lasema taarifa inayosambaa sio ya kweli na ipuuzwe.
- Mpaka sasa haijulikani kama Lissu yupo gereza la Keko au la.
Dar es salaam. Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazosambaaa katika mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Jeshi la Magereza la Tanzania limetolea ufafanuzi juu ya taarifa zinazohusiana na kuhamishwa gereza kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu ambaye kwa sasa anashikiliwa na Jeshi hilo kwa tuhuma zinazomkabili. Taarifa hizo si za kweli na zinapaswa kupuuzwa.
Taarifa hiyo inayosambaa katika mitandao ya kijamii hasa mtandao wa X huku baadhi ya vyombo vya habari vikiripoti inaonekana kama chapisho rasmi la taarifa kwa umma kutoka Jeshi la Magereza likiwa na nembo ya jeshi hilo na sahihi ya Msemaji wa Jeshi hilo, Elizabeth Mbezi.
Chapisho hilo ghushi linaeleza kuwa Lissu ambaye kesi yake inaendelea kusikilizwa mahakamani bado anaendelea kushikiliwa katika Gereza la Keko, ikikanusha uvumi unaosambaa kwenye mitandao kuwa mtuhumiwa huyo amehamishwa gerezani hapo kwa siri na kupelekwa mahala pasipo julikana pasipo wakili wake na watu wa karibu kupewa taarifa.
“Mheshimiwa Lissu bado yupo salama na anaendelea kushikiliwa na katika gereza la keko, Dar es Salaam kwa mujibu na sheria za nchi” linasomeka chapisho hilo.
Pia chapisho hilo linaeleza kuwa watu wote wanaotaka kumtembelea au kumuona mtuhumiwa huyo wafuate taratibu rasmi zilizowekwa, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana mapema na uongozi wa Gereza la Keko kwa ajili ya kupata kibali na kufuata masharti yanayohitajika.
Jeshi la Magereza kupitia akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii, limekanusha taarifa hizo na kusema kuwa chapisho hilo ni batili na halikutolewa na Jeshi hilo hivyo umma unapaswa kupuuza.
Hata hivyo, ingawa Jeshi la Magereza limekanusha taarifa hiyo, bado halijatoa ufafanuzi ikiwa ni kweli Lissu amehamishwa au lah!
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema Aprili 18, 2025 kupitia msemaji wake Brenda Rupia inaeleza kuwa vingozi wa chama hiko akiwemo Katibu Mkuu Chadema, Zanzibar, mawakili pamoja na wanafamilia wa Lissu walifika katika Gereza la Keko kwa nyakati tofauti ili kumuona mtuhumiwa huyo lakini juhudi za kumona hazikuzaa matunda baada ya kuelezwa kuwa mtuhumiwa hayupo katika gereza hilo huku kukiwa hakuna taarifa yeyote juu ya mahali alipopelekwa.
Aidha, katika mahojiano yake ya hivi karibuni na Jukwaa la Habari la Jamii Forum, msemaji wa Jeshi la Magereza Elizabeth Mbezi alipoulizwa ikiwa kama kuhamisha watuhumiwa na wafungwa hufanyika kwa siri amesema kuwa usiri juu ya uhamishwaji wa mtuhumiwa au mfungwa hutegemea aina ya makosa yanayomkabili mhusika akifafanua kuwa yapo makosa ambayo huhamishwa kwa siri na yapo ambayo hawahamishwi kwa siri.
Aikijibu swali kuhusiana ukweli wa taarifa zinazosambaa mitandaoni juu ya kuhamishwa kwa mtuhumiwa Lissu alitoa majibu ya kuwa hajui mpaka afuatilie. Limeripori Jukwaa la Habari Jamii Forum.
Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi Aprili 9, 2025 alipokuwa katika mkutano wa kisiasa wa chama chake mkoani Ruvuma ambapo kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani humo Marco Chillya, mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa tuhuma za kufanya uchochezi wa kutofanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mara ya kwanza Lissu alifikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Aprili 10, 2025. Mpaka sasa bado anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama huku kesi yake ikiwa inaendelea kusikilizwa mahakamani ambapo inatarajiwa kusikilizwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24, 2025.
Latest



