Chadema kutoshiriki uchaguzi kwa miaka mitano Tanzania

April 12, 2025 3:54 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima amesema Chadema ambayo haikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, haitashiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.

Kanuni hizo zimesainiwa leo Aprili 12, 2025 na vyama vya siasa 18 vyenye usajili wa kudumu, Serikali na (INEC) jijini Dodoma ambapo Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu wake John Mnyika walitangaza kutoshiriki tukio hilo kupitia kurasa za mitandao ya kijamii.

“Chama cha Chadema ambacho hakikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025, hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.” ameeleza Ramadhan wakati wa mahojiano na waandishi wa habari.

Ramadhani amesisitiza kuwa kanuni hizo zimeundwa kuhakikisha uchaguzi wa haki na uwazi, na vyama vyote vilivyosajiliwa kudumu vinapaswa kuziheshimu.

Awali, Mwenyekiti wa INEC Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amesisitiza umuhimu wa kila chama cha siasa na kila mgombea kuhakikisha wanasaini na kuzingatia kanuni za maadili ya uchaguzi kabla ya kuwasilisha fomu za uteuzi, kama inavyotakiwa na sheria. 

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni ya lazima kwa mujibu wa Kifungu cha 162 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024, na inalenga kuhakikisha kuwa wadau wote wa uchaguzi wanazingatia misingi ya kimaadili wakati wa kampeni na uchaguzi kwa ujumla. 

Hata hivyo, taarifa ya Chadema imebainisha kuwa msimamo huo umetokana na kutokuwepo kwa majibu ya maandishi kutoka (INEC) kuhusu barua rasmi iliyowasilishwa na Katibu Mkuu Desemba 29, 2024 akieleza mapendekezo na madai ya msingi ya Chadema kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.

“Ukimya huu unathibitisha kukosekana kwa nia ya dhati ya kufanya mashauriano ya kweli na ya wazi kuhusu mchakato wa uchaguzi,” inaeleza taarifa ya Chadema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks