Sh91.8 bilioni: Hasara yazidi kuiandama Air Tanzania
- Yarekodi hasara ya Sh91.8 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 ndani ya mwaka mmoja.
- Rais Samia asema Serikali itafanyia kazi mapendekezo.
Arusha. Licha ya Serikali kuiimarisha kampuni ya ndege ya Air Tanzania, kampuni hiyo bado imeendelea kuandamwa na hasara baada ya kuripoti hasara ya Sh91.8 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2023/24 ikichochewa zaidi na gharama kubwa za matengenezo ya ndege.
Hasara hiyo iliyoripotiwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2024, ni ongezeko la asilimia 62 ndani ya mwaka mmoja kutoka Sh56.6 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2022/23.
Katika miaka mitatu iliyopita Air Tanzania ilikuwa ikipunguza kiwango cha hasara mwaka hadi mwaka kiasi cha kutoa matumaini kuwa huenda ingeanza kuripoti faida baada ya miaka mingi ya kukosa ufanisi.
Mwaka 2021/22 ATCL ilianza kuonesha matumaini ya kuimarika baada ya hasara kupungua kwa Sh1 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja huku kukiwa na ongezeko la safari kwenda mataifa mbalimbali na kuongezeka kwa wasafiri wa ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, matumaini hayo yalianza kufifia mwaka mmoja baadae baada ya shirika hilo kutengeneza hasara ya Sh56.6 bilioni iliyoongezeka kutoka Sh35 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2023.
“Hasara hii ilitokana na gharama kubwa za matengenezo ya ndege na hitilafu za injini ambapo ndege za Airbus zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi zikisubiria injini,” amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) CAG Charles Kichere wakati akiwasilisha muhtasari wa ripoti za ukaguzi za hesabu za Serikali.
Bila ruzuku hasara ingekuwa balaa
Kichere ameeleza kuwa katika mwaka huo wa fedha wa 2023/24 Air Tanzania ilitumia Sh99.8 bilioni kukidhi gharama za uendeshaji zilizotolewa na Serikali kama ruzuku.
Bila ruzuku hiyo, Kichere ameeleza leo Machi 27, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa hasara halisi ya Air Tanzania ingefikia 191.6 bilioni ndani ya mwaka huo wa fedha, kiwango ambacho kingekuwa mara tatu zaidi ya hasara ya mwaka 2022/23.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/24 kutoka kwa Charles Kichere kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.Picha/Ikulu.
Ruzuku hiyo ni sehemu ya uwekezaji wa mabilioni ya fedha ambao Serikali imekuwa ikiufanya ATCL tangu mwaka 2016 ili kuifufua baada ya kuyumba vibaya sokoni kwa miaka iliyopita.
Mpaka sasa ATCL ina jumla ya ndege 16 ikiwemo ndege ya mizigo ya Boeing 767-300F ambayo imechangia kupaisha usafirishaji wa mzigo ndani na nje ya nchi na kufikia tani zaidi ya 6,000.
“Napendekeza kampuni, Shirika na Serikali kufanya utafiti kuhusu njia nzuri zaidi za uendeshaji wa ndege kwa kuzingatia masuala ya kifedha na kiuchumi ili kuongeza ufanisi wa kiundeshaji,” amesema Kichere.
Samia aahidi kushughulikia mapendekezo
Hata hivyo, Air Tanzania imekuwa ikikosolewa vikali na baadhi ya watumiaji wakilalamika kuwa sehemu ya safari ndani na nje ya nchi hucheleweshwa mara kwa mara jambo linalowakwamisha malengo yao.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akipokea ripoti hiyo amesema ukaguzi uliofanyika unatoa taswira ya matokeo katika kuziimarisha taasisi za umma nchini ili ziweze kutumia vizuri rasilimali za Serikali.
“Niseme tu ripoti nimeipokea na mimi nitaifikisha bungeni haraka iwezekanavyo na mapendekezo yaliyotolewa tutafanyia kazi,” amesema Rais Samia.
Latest



