Majaliwa: Mafunzo ya Veta ni  muhimu katika kutengeza ajira, kukuza uchumi

March 18, 2025 3:42 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Majaliwa asema mafunzo ya ufundi yaliwezesha vijana milioni 7.1 kujiajiri mwaka 2020 mpaka 2024.
  • Vyuo vya Veta 65 kujengwa katika wilaya na mikoa yote nchini.

Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo mbalimbali nchini ikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) ni muhimu katika kutengeneza ajira na kukuza uchumi.

Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2025 amesema kutokana na ukosefu wa ajira uliopo hivi sasa mafunzo hayo ni kimbilio pekee la vijana katika kujipatia ajira.

“Mwenendo wa kidunia unaonesha wazi kuwa mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu katika kutengeneza fursa za ajira na kukuza uchumi wa nchi yoyote ile…

…Hivyo wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi wana fursa kubwa ya kupata ajira au kujiari hasa katika sekta isiyokuwa rasmi ambayo inahitaji stadi maalum za kiufundi,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Kasssim Majaliwa (kulia) akitazama baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na Watanzania katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta,Picha|VPMO.

Kauli ya Majaliwa inakuja ikiwa bado kuna maoni mseto katika jamii na mitandao ya kijamii kuhusu kauli aliyoitoa hivi karibuni ya wahitimu wa ngazi ya shahada kujiunga na Veta ili kujiongezea ujuzi na kujipatia ajira.

Hiyo imetokana na wimbi kubwa la vijana wanaohitimu masomo hayo ya ngazi ya juu kuendelea kusota mtaani wakisubiri ajira za Serikali na sekta binafsi ambazo ni chache kulinganisha idadi ya wahitimu hao.

Ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania (Tanzania in Figure 2023) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inabainisha kuwa kiwango cha vijana wasio na ajira Tanzania mwaka 2023 kilikuwa asilimia 9 kikipungua kidogo kutoka asilimia 8.9 mwaka 2022.

Pamoja na ukosefu huo wa ajira, Majaliwa amesema kuwa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinazonesha asilimia 70 ya ajira zote duniani zinatokana na ufundi stadi huku nchini Tanzania watu milioni 7.1 wakijiajiri ama kuajirwa kutokana na ufundi huo ndani ya miaka minne iliyopita

“Takwimu za ajira zilizozallishwa kati ya mwaka 2020 mpaka 2024 zimefikia milioni 7.1 ambapo ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi ni milioni 6.1 sawa na asilimia 87 ambapo wengi wao wana elimu ya ufundi stadi,”amesema Majaliwa.

Ili kuendelea kuongeza idadi ya vijana wa Tanzania watakaonufaika na sekta hiyo, Majaliwa amesema Serikali inajenga vyuo vya Veta 65 katika wilaya na mikoa yote nchini na kufanya jumla ya vyuo hivyo kufikia 145.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema mbali na ujenzi wa vyuo hivyo, Serikali imefanya maboresho ya Sera ya Elimu ambapo wanafunzi watapata mafunzo ya ufundi kabla hawajamaliza kidato cha nne.

Pamoja na hayo, amewataka wafadhili kutoka ndani na nje ya nchi kuendelea kujitokeza ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi hususani wasiokuwa na uwezo kupata mafunzo hayo yatakayowawezesha kujiajiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks