Rais Samia azindua miradi ya maendeleo ziarani Tanga
- Ni pamoja na uzinduzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli pamoja na uwekwaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa bwawa la Mkomazi.
Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa bwawa la Mkomazi unaotajwa kuchochea kilimo jijini Tanga.
Rais Samia ambaye yuko ziarani kwa wiki moja jijini humo leo Februari 24, 2025 ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Bumbuli, Lushoto na Korogwe akizungumza na wananchi pamoja na kuzindua miradi hiyo.
Akizungumza baada ya kuzindua bwawa la Mkomazi Rais Samia amesema “Lengo letu mabwawa haya yatumike kwa kilimo, yatumike kwa mambo mengine pia lakini kubwa ni uzalishaji wa mazao ya kilimo… tunakwenda kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kilimo, Mwalimu Nyerere alisema kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa letu, tunakwenda kulithibitisha hilo”

Kwa mujibu wa Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Tanga, Leonard Someke, bwawa hilo lina ukubwa wa hekta 1,469 na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo bilioni 17.5 za maji.
Bwawa hilo linatarajiwa kutumika kwa umwagiliaji wa hekta 9,000 katika vijiji 29 vya Wilaya ya Korogwe, hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao na kuinua kipato cha wakulima wa eneo hilo.
Mpaka sasa ujenzi wa Bwawa hilo umefikia asilimia 30 na linatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 huku likitarajiwa kuleta tumaini jipya kwa wakulima wa eneo hilo likiwahamisha kutoka kilimo cha kutegemea mvua hadi kilimo cha umwagiliaji.
Rais Samia pia amezindua jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, akisisitiza umuhimu wa miundombinu bora kwa watumishi wa umma na wananchi.

“Jengo hili ni la wananchi wa Bumbuli. Huduma zote zitapatikana hapa, na naomba mlitumie kwa manufaa yenu. Lengo letu ni kuboresha huduma kwa wananchi na kutoa fursa kwa watumishi wetu kufanya kazi zao kwa ufanisi,” amesema Rais Samia.
Changamoto ya barabara, wanyama pori kutatuliwa
Aidha, Rais Samia ametumia ziara hiyo kusikiliza changamoto za wakazi wa wilaya ya Bumbuli na Lushoto ikiwemo wanyamapori kuharibu mazao ya wakulima.
“Nataka nimuagize Waziri wa Utalii aone uwezekano wa kufanya mapitio ya kanuni za fidia kwa wale ambao wanaingiliwa kwenye mashamba yao,” amesema Rais Samia.
Rais Samia pia ameweka wazi hatua za kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa wa Tanga. Amesema tayari serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Soni–Bumbuli–Korogwe pamoja na barabara ya Tanga–Bagamoyo kupitia Pangani.
“Nataka niwaambie tarehe sita mwezi ujao tunafungua tenda kutafuta mkandarasi na barabara itaanza kujengwa,” alitangaza Rais Samia.
Barabara hiyo itajengwa kwa urefu wa kilomita 22 kutoka Soni kuelekea Bumbuli, na kilomita 9.3 kutoka Kwa Meta hadi Kwa Shemsi.
Latest



