Tanesco: Maboresho miundombinu kuathiri upatikanaji umeme Dar, Zanzibar na Pwani
- Wakazi wa maeneo husika washauriwa kuchukua tahadhari kwa kupanga matumizi yao ya umeme kuepuka usumbufu.
Dar es Salaam, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema mikoa ya Zanzibar, Dar es Salaam, na Pwani itakosa umeme kwa nyakati tofauti kati ya Februari 22 na 28, 2025 kutokana na maboresho ya miundombinu katika kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tanesco Jumatano, Februari 19, maboresho hayo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo za kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kufuatia ongezeko la mahitaji ya umeme katika maeneo hayo.
“Hatua hii ni muhimu kwa shirika katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake kufuatia ongezeko la mahitaji ya matumizi ya umeme,” taarifa hiyo imeeleza.
Shirika hilo limeeleza kuwa moja ya sababu kuu za kukosekana kwa umeme ni kufungwa kwa mashineumba (transformer) mpya yenye uwezo wa MVA 300 katika kituo cha Ubungo, baada ya kituo hicho kuzidiwa na mahitaji ya umeme.

Hata hivyo, Tanesco imewahakikishia wananchi kuwa maboresho hayo hayatakuwa kwa siku sita mfululizo na hayatawaathiri wananchi kwa muda wote.
Aidha, wakati wa maboresho hayo, Tanesco pia itafanya matengenezo ya miundombinu ya umeme katika maeneo husika ili kuimarisha mifumo yake hasa kuelekea msimu wa mvua.
Tanesco pamoja na kuomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza imeahidi kuendelea kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya kazi hiyo mpaka itakapokamilika.
Miongoni mwa athari zinazotarajiwa ni kuathirika kwa shughuli zinazotegemea upatikanaji wa umeme kwa kiasi kikubwa kama za viwanda vidogo na vikubwa, uhifadhi wa vyakula na vinywaji pamoja na uwezeshaji wa huduma za kijamii kama maji.
Wananchi wa Zanzibar, Dar es Salaam, na Pwani wanashauriwa kuchukua tahadhari kwa kupanga matumizi yao ya umeme kwa kuzingatia muda wa matengenezo hayo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Latest



