Wakuu wa nchi EAC, SADC waazimia kusitishwa kwa mapigano DRC

February 8, 2025 6:59 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema vita haiwezi kumaliza mgogoro huo badala yake watumie mbinu ya majadiliano
  • Wakuu wa majeshi EAC,SADC wapewa maagizo mazito.

Arusha. Wakuu wa nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameazimia kusitishwa mara moja kwa mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Wakuu hao wa nchi waliokutana leo Februari 8, 2025 kwa ajili ya kutafuta suluhu ya vita inayoendelea kwa takribani wiki mbili katika mji wa Goma, uliopo mashariki mwa DRC wamekubaliana masuala makubwa matatu ikiwemo kutumia majadiliano ya kidiplomasia kutatua mgogoro huo.

“Baada ya kujadili hali ya usalama mashariki mwa DRC, mkutano ulitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na usitishaji wa mapigano mara moja…

…Mkutano umezingatia ripoti ya mkutano wa pamoja wa mawaziri wa EAC na SADC kuhusu hali ya usalama mashariki mwa DRC na kusisitiza kwamba mazungumzo ya kidiplomasia ndilo suluhisho endelevu zaidi kwa mgogoro huo,”amesema Veronika Nduva, Katibu Mkuu EAC akiwasilisha maazimio hayo.

Mbali na maazimio hayo  wakuu hao wa nchi pia wameazimia kurejeshwa kwa huduma muhimu na njia za usambazaji wa chakula na bidhaa nyingine muhimu ili kuhakikisha msaada wa kibinadamu na utatuzi wa amani wa mgogoro kupitia mchakato wa Luanda na Nairobi.

Awali Mwenyekiti wa EAC na Rais wa Kenya William Ruto alisema kuwa mgogoro huo hauwezi kutatuliwa kwa kutumia mitutu katika uwanja wa vita ila mbinu bora za kidiplomasia ndiyo zinaweza kumaliza mzizi wa tatizo.

“Nina uhakika mtakubaliana namimi kuwa mazungumzo si dalili ya udhaifu bali ni ishara ya nguvu… Kujadiliana kwa kina kwa nia thabiti na kwa uvumilivu huleta suluhisho bora,” amesema Ruto.

Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa hali inayoshuhudiwa mashariki mwa DRC haikubaliki na ipo haja ya kuchukua hatua za haraka kumaliza mgogoro huo unaoleta mateso kwa  wananchi.

Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu ya vita inayoendelea DRC ikulu jijini Dar es Salaam. Picha Ikulu.

Maagizo kwa wakuu wa majeshi EAC na SADC

Mkutano huo pia umetoa maagizo kwa  wakuu wa majeshi wa EAC na SADC kukutana ndani ya siku tano na kutoa mwelekeo wa kiufundi kuhusu kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti, utoaji wa msaada wa kibinadamu ikiwemo urejeshaji wa miili ya marehemu na uokoaji wa majeruhi.

Aidha, wametakiwa kuandaa mpango wa usalama kwa Goma na maeneo jirani, kufunguliwa kwa njia zote kuu za usambazaji zikiwemo Goma-Sake-Bukavu, Goma-Kibumba-Rumagambo-Kalegera, Rutsuru-Bunagana.

Maeneo mengine yanayotakiwa kufunguliwa ni pamoja na Goma-Kiwanja-Rwindi-Kanyabayonga-Nyonga-Lubero, na kuimarishwa kwa usafiri wa majini kwenye Ziwa Kivu kati ya Goma na Bukavu huku wakitakiwa pia kufungua wanja wa ndege wa Goma mara moja na kutoa ushauri kuhusu hatua nyingine zinazosaidia.

Ikiwa maazimio hayo yatafanyiwa kazi huenda vita ya takribani miongo mitatu inayoikabili DRC ikafikia ukomo ikitoa nafasi kwa wanachi kuishi kuwa na amani na utulivu utakaowawezesha kushiriki shughuli mbalimbali za uchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks