Serikali yatoa muongozo kwa wasafiri kudhibiti Marburg

January 23, 2025 5:25 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kujaza fomu maalumu ya ufuatiliaji wa hali ya afya huku wale waliopo katika hatua ya ufuatiliaji kutoruhusiwa kusafiri.
  • Mwongozo huo utahuishwa kadri itakavyohitajika.

Arusha. Serikali ya Tanzania imetoa mwongozo kwa wasafiri wa safari za ndani na nje ya nchi utakaosaidia kudhibiti ugonjwa wa Marburg na kuzuia kusambaa katika maeneo mengine.

Muongozo huo unakuja ikiwa ni siku mbili tangu Tanzania iripoti mgonjwa wa kwanza wa Marburg katika mkoa wa Kagera huku Serikali kupitia Wizara ya Afya na mashirika ya kimataifa ikiahidi kuanza hatua za haraka kuudhibiti.

Taarifa ya Seif Shekilage, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya iliyotolewa Januari 22, 2025 inabainisha kuwa mwongozo huo utaanza kutumika mara mora moja ukihusisha wasafiri wote wa ndani na nje ya mkoa wa Kagera.

“Serikali ya imeimarisha hatua za kudhibiti mlipuko huo ili kuzuia kusambaa ndani na nje ya nchi kulingana na kanuni za afya za Kimataifa za mwaka 2005…

….Serikali imeandaa Mwongozo Na. 15 wa tarehe 21 Januari 2025 kwa wasafiri kuhusiana na ugonjwa huu utakaoanza kutumika mara moja ili kutekeleza hatua madhubuti zinazohusiana na safari za ndani na za kimataifa, imesema taarifa ya Shekilage.

Mwongozo huo unawataka wasafiri wote kutoka Mkoa wa Kagera kujaza kwa uaminifu fomu ya ufuatiliaji wa hali ya afya ya wasafiri iliyopo katika mtandao kwa anuani https://afyamsafiri.moh.go.tz huku wale waliopo katika hatua ya ufuatiliaji kutoruhusiwa kusafiri.

Kundi hilo litaruhusiwa kusafiri nje ya mkoa wa Kagera au nje ya nchi pale wataalamu wa afya watakapomaliza kipindi cha ufuatiliaji na kuruhusiwa.

Mwongozo mwingine utahusisha mipaka ya nchi ikiwemo viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu au bandari ambapo wasafiri wote watapimwa joto la mwili na watakaobainika kuwa na homa watafanyiwa uchunguzi wa kina na mamlaka za afya mipakani.

Pia Wizara ya Afya itatoa elimu kuhusu  utoaji wa taarifa mapema na ushauri wa afya kuhusu kuripoti dalili zozote za ugonjwa wa Marburg vitatolewa kwa wasafiri wote mipakani au kwa kupitia namba ya bure ya simu 199.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma baada ya kutangaza mgonjwa wa kwanza kuathirika na Marburg Tanzania Januari 20, 2025.Picha|Ikulu Mawasiliano.

Wale watakaoonesha dalili hizo watafanyiwa uchunguzi wa kina na kupatiwa matibabu katika vituo vya huduma za afya.

Aidha, wasafiri wote na wafanyakazi mipakani wanatakiwa kuzingatia hatua za kujikinga na kudhibiti maambukizi kama vile kunawa mikono au kutumia vitakasa mikono (sanitizer), kuepuka misongamano inayosababisha kugusana na kuripoti dalili yoyote kwa kutumia namba ya bure ya simu 199.

Katika hatua nyingine wasimamizi wote wa vyombo vya usafiri na madereva wanapaswa kufuata hatua za uchunguzi mipakani huku wakizingatia usafi ikiwemo kunawa mikono.

 Madereva wanapaswa kuzingatia hatua za uchunguzi ikijumuisha uchunguzi wa afya, ukaguzi wa usafi wa vyombo vya usafiri, kunawa mikono, matumizi ya vitakasa mikono, na kutoa taarifa mara moja kuhusu msafiri yeyote mwenye dalili zozote kwa mamlaka za afya mipakani.”imesema taarifa ya Shekilage.

Pamoja na taarifa hiyo, Wizara ya Afya imesema mwongozo huo wa wasafiri utakuwa ukihuishwa mara kwa mara kadri itakavyohitajika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks