Imani Henrick: Mafunzo yamenifanya niwe mtangazaji bora
Meneja Programu wa televisheni ya Crown (Crown TV), mwanzilishi wa podicasti ya ‘Dig It With Imani’
Dar es Salaam. Akiwa katika masomo ya sekondari alitamani kuwa mwanasheria mbobevu. Ndoto yake haikutimia kama alivyotarajia pale alipojiunga chuo kikuu baada ya kujikuta akibadili mwelekeo wa taaluma yake. Uanasheria wake ulibaki ndotoni tu.
Huyu ni Imani Henrick, Meneja Programu wa televisheni ya Crown (Crown TV), mwanzilishi wa podicasti ya ‘Dig It With Imani’ na mkufunzi wa masuala ya haki za kidijitali nchini Tanzania. Binti huyu ni miongoni mwa vijana mashuhuri katika uhamasishaji wa matumizi ya kidijiti nchini.
“Kilichonivutia kuingia katika tasnia ya habari ni kuwaona wanahabari hasa wale wa zamani. Mimi nilikuwa namtazama sana Rehema Mwakangale. Nilikuwa napenda vile anavyosoma habari, nilikuwa navutiwa natamani kuwa kama yeye lakini nilikuwa sijui nitakuwa kama yeye,” anasema Imani.
Kujiunga kwake katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano Kwa Umma ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (SJMC-UDSM) mwaka 2019 na motisha ya baadhi ya watu wakiwemo walimu ilikuwa fursa muhimu ya kumjenga katika taaluma hiyo.
Katika shule hiyo iliyopo Dar es Salaam, kuna vyombo vya habari vinavyotumika kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho kikongwe nchini.
“Kuna siku tuliambiwa kaeni hapa jaribuni kutangaza, sasa yule aliyekuwa anatusimamia akanisifia sana akasema nina sauti nzuri na una mwonekano wa kutangaza habari,” anasema Imani.
“Basi ndoto ya kuwa mwanasheria ikaishia pale, nikaendelea kujifunza na kuipenda hii kazi ya uandishi wa habari.”
Imani, ambaye pia anafanya kazi na Shirika la Utangazaji la Deutsche Welle (DW) la Ujerumani, alianza kuandaa mazingira ya kufanikiwa tangu akiwa chuoni kwa kuzisaka fursa za mafunzo nje ya masomo ya darasani.
Anasema kampuni ya Nukta Africa ni miongoni mwa taasisi za mwanzo ambazo zilimuonyesha namna ya kufanikiwa katika tasnia ya habari kupitia programu zake mafunzo zinazotoa ujuzi wa kisasa katika habari na mawasiliano.
Anasema Nukta Africa ina mchango mkubwa katika taaluma yake ambayo siyo tu imemfanya kuwa mtangazaji maarufu bali mzalishaji maudhui ya mtandaoni na mkufunzi na mhamasishaji wa haki za kidijitali ikiwemo uhuru wa kujieleza.
Nukta Africa ni kampuni ya habari na teknolojia iliyojikita katika kufanya utafiti wa masuala ya kisasa ya habari na mawasiliano, utoaji wa mafunzo ya ujuzi wa kisasa katika habari na mawasiliano na uzalishaji wa maudhui ya takwimu na kidijiti.
Imani Henrick, Meneja Programu wa televisheni ya Crown (Crown TV). Picha | Imani Henrick.
Akiwa mwaka wa pili wa masomo yake UDSM, Imani alikuwa miongoni mwa waandishi wa habari 20 wa Tanzania ambao walipata mafunzo ya miezi sita ya kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa usahihi habari za nishati jadidifu (Renewable Energy Fellowship).
Mafunzo hayo ya nadharia na vitendo yaliendeshwa na Nukta Africa kwa ushirikiano na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Hivos East Africa mwaka 2019/2020 yakilenga kuwawezesha wanahabari kubobea katika uandishi wa habari za nishati jadidifu kwa kutumia mbinu za kisasa ikiwemo matumizi ya takwimu na multimedia storytelling.
“Nukta Africa ilikuwa mkombozi katika taaluma yangu kwa sababu nilikuwa mchanga, nimefanya mafunzo ya uthibitishaji habari na nishati jadidifu nikiwa mwaka wa pili na yalikuwa mafunzo yangu ya kwanza ya muda mrefu,” anasema Imani na kuongeza kuwa “Unapojua unataka nini unatafuta ujuzi wa kukuboresha zaidi.”
Washiriki wa mafunzo hayo walipata pia fursa ya kukutanishwa na wataalamu mbalimbali wa nishati, kutembelea miradi ya nishati jadidifu na kufanya mahojiano na wananchi ili kuongeza uelewa na kuwafikia watu wengi kwa habari sahihi za redioni, magazetini, televisheni na mtandaoni.
‘Mafunzo yalibadili maisha yangu’
Imani anasema kuaminiwa kuingia katika mafunzo hayo wakati bado ni mwanafunzi ilikuwa ni jambo ambalo hakulitegemea na alimlazimu kuitumia fursa hiyo vizuri ili kufikia malengo yake.
Uwepo wa redio Mlimani FM na Mlimani TV ya UDSM ulizidi kumnoa zaidi na kuyatendea kazi maarifa na ujuzi alioupata kwenye mafunzo hayo ya miezi sita kuhabarisha umma kwa habari bora na zilizohakikiwa.
Ujuzi alioupata katika mafunzo hayo ni pamoja na uandishi wa habari za takwimu, uthibitishaji habari, multimedia storytelling na kubobea katika habari za nishati, japo kwa sasa amejikita katika kufundisha na kuripoti kuhusu haki za kidijitali.
Nukta Africa siyo tu imemfungulia Imani dunia ya tasnia ya habari, pia kupitia mafunzo yake imemkutanisha na wadau mbalimbali kujenga mahusiano endelevu na kupata ujuzi wa kuongoza watu na taasisi za vyombo vya habari.
Mathalan, alipohitimu masomo yake mwaka 2022 aliajiriwa kuwa Mkuu wa Kituo cha Redio cha Kings FM cha mkoani Njombe ambako huko ameacha alama isiyofutika ya kuikiimarisha kituo hicho kiutendaji na kimapato.
Imani Henrick pia ni mkufunzi wa masuala ya haki za kidijitali na usawa wa kijinsia. Picha | Imani Henrick.
‘Pale ni nyumbani’
“Kuna knowledge (maarifa) nyingi ambazo nazitumia ambazo nimejifunza kutoka Nukta. Hata nikikwama mambo ya data narudi tena nyumbani. Nayatumia mafunzo kutoka Nukta Africa kuwasisitiza wanahabari kuhakiki habari kama ni za ukweli, kutumia takwimu lakini kubwa zaidi mpangilio wa makala ile sanaa ya kusimulia habari,” anasisitiza Imani.
Mafunzo mengine ambayo amewahi kupata kutoka Nukta Africa ni ya uandishaji wa habari za takwimu na uthibitishaji wa habari ambayo yalitolewa kwa pamoja na Internews Tanzania.
Imani anaishauri Nukta Africa, inayomiliki maabara ya Nukta Lab na jukwaa kujifunza la mtandaoni la Kozica kuendelea kutoa mafunzo ya ujuzi wa kisasa katika habari na mawasiliano kwa sababu una manufaa makubwa kwa waandishi wa habari.
Pia anawashauri wakufunzi waendelee kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kufahamu utekelezaji wa ujuzi wanaowapatia washiriki wa mafunzo huku ikiendelea kufanya tafiti za ujuzi mpya anaoweza kuwasaidia waandishi habari kuboresha kazi zao.
“Nipende kuishukuru Nukta Africa mnafanya kazi nzuri sana, mmetusaidia waandishi habari kutuamsha usingizini. Mnahitaji kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa waandishi wanaendeleaje na kuangalia namna ya kuwafikia wanahabari ambao bado hawajafikiwa,” anashauri Imani.
Mpaka sasa, Nukta Africa yenye makao yake jijini Dar es Salaam imetoa mafunzo kwa watu wasiopungua 3,000 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018.
Kama unapenda kuongeza ujuzi wa namna ya kutumia takwimu, kuthibitisha habari, kutengeneza maudhui ya mtandaoni yenye matokeo makubwa, usisite kuwasiliana nasi kupitia baruapepe trainings@nukta.co.tz au simu: 0677088088.