Mganga Mkuu wa Serikali atwishwa zigo kupambana na magonjwa ya mlipuko Tanzania
- Ni baada ya kuripotiwa mgonjwa wa kwanza wa Marburg Tanzania.
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe kudhibiti ueneaji wa magonjwa ya mlipuko nchini ili kupunguza hatari za vifo pamoja na nchi kuwekewa vikwazo na nchi za kimataifa.
Hayo yamejiri ikiwa ni siku mbili tangu Tanzania iripoti mgonjwa wa kwanza Marburg, nkoani Kagera huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likiahidi kutoa ushirikiano ikiwemo wa kifedha kupambana na ugonjwa huo.
Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati akiwaapisha majaji wanne wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa Januari 10 mwaka huu pamoja na viongozi wengine huku akimsisitiza Dk Grace kushirikiana na watumishi wengine kupambana na magonjwa hayo.
“Sasa naomba haya mambo ya mlipuko mlipuko yanayotokea ndani ya nchi yetu uende ukaisimamie vyema wewe na timu yako, ni imani yangu kuwa utafanya kazi yako kama unavyotakiwa kuifanya…
…Na kuiepusha nchi yetu kuingizwa kwenye ma-alert (tahadhari) na kusimishwa kwenye usafiri na mambo mengine kama hayo,” amesema Rais Samia leo Januari 22, 2025 ikulu Jijini Dodoma.
Dk Grace anakabidhiwa majukumu hayo akiwa na siku tano tangu ateuliwe kuwa Mganga Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Prof Tumaini Nagu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Samia Januari 17 mwaka huu.
Mbali na jukumu la kupambana na ugonjwa wa Marburg Dk Grace anakabiliwa na jukumu la kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu jijini Mbeya ambapo hadi kufikia Januari 8, 2025 wagonjwa walifikia 261 kwa mujibu wa taarifa ya Mganga Mkuu wa jiji hilo Dk Yesaya Mwasubila.
Mbali na maagizo hayo, Rais Samia amewapongeza majaji hao walioapa leo kwa kuteuliwa katika nafasi hizo huku akiwataka kufanya kazi kwa weledi.
“Ni imani yangu kwamba mtawenda kufanya kajukumu wajibu unaotakiwa kama tunavyojua jukumu la utoaji wa haki nchini kwa mujibu wa ibara ya 107a lipo mikononi mwa mahakama kwa mujibu wa katiba yetu,
Kwa upande wake Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amemshukuru Rias Samia kwa uteuzi huo ambao umefanya jumla ya majaji wa rufani kuwa 39 ambao watasaidia kuharakisha utoaji wa hukumu na kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani
“Uwezeshaji huu umetusaidia kupunguza mlundikano wa mashauri na kuondoa msongamano magereza…uwezo wa kubeba maabusu na wafungwa hadi mwezi Novemba kulikuwa na wafungwa 29,000 lakini hivi sasa wamepungua kuna nafasi 2,000 za kujaza,” amesema Prof Juma.