Jinsi madereva daladala, mabasi  wanavyoweza kuepuka maumivu ya mgongo

January 14, 2025 3:57 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na kukaa muda mrefu kwa zaidi ya masaa 10
  • Wataalamu wa afya waeleza suluhu.

Arusha. Harakati za maisha huwafanya watu kuchagua kazi au shughuli ya kufanya inayowaingizia kipato kinachowasaidia kumudu gharama za maisha.

Lakini je? Utafanyaje pale ambapo kazi unayoifanya inageuka kuwa chanzo cha maumivu ya kudumu katika mwili wako

Hiyo ndiyo hali wanayokutana nayo madereva wa mabasi na daladala ikiwemo za mkoani Arusha ambao hufanya kazi kwa zaidi ya saa 10 jambo linalowasababishia maumivu ya mgongo.

James kirway (28) ni dereva wa daladala za Morombo Arusha anasema kwa zaidi ya miaka nane aliyokuwa akifanya kazi hiyo amekuwa akikumbana na matatizo ya mgongo bila kupata suluhu ya kudumu.

“Hii ‘ishu’ ya mgongo ni kila siku tunapambana nayo kama unaamka saa11 alfajiri na kurudi nyumbani saa tatu au saa nne usiku unaachaje kuumwa? Amesema Kirway.

Kirway ni miongoni watu milioni 619 ambao Shirika la Afya Duniani {WHO) linawakadiria kukutana na tatizo hilo mwaka 2020 duniani kote, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi mwaka 2050.

Maumivu ya mgongo wa chini (LBP) ndiyo sababu kuu ya ulemavu duniani kote…Inakadiriwa kuwa idadi ya visa itaongezeka hadi kufikia milioni 843 ifikapo mwaka 2050, hasa kutokana na ongezeko la idadi ya watu na uzee.” imesema WHO.

Baadhi ya abiria wakipanda na kushuka katika daladala katika stendi ya kona ya dampo jijini Arusha.Picha Lucy Samson.

Kirway huianza siku yake saa 11 alfajiri akichukua abiria morombo hadi stendi ndogo jijini Arusha na hurudia safari zake mara tatu au nne kabla ya kupumzika kidogo kwa ajili ya kupata chai ambapo wakati mwingine hulazimika kuinywa akiwa kwenye gari ikiwa abiria ni wengi.

Baada ya chai ya asubuhi safari huendelea akiendesha gari umbali wa kilomita 16 kwa kila ruti mpaka pale watakapopumzika tena kwa muda kidogo kupata chakula cha mchana.

“Wakati wa mchana kama huu kunakuwaga hamna abiria kwa hiyo tukila tunapumzika kama hivi ndipo ninapopata nafasi ya kupumzisha mgongo kisha kazi inaendelea.” amesema Kirway.

Mapumziko hayo yanayochukua hadi saa moja yakiisha Kirway pamoja na kondakta wake huendelea kusafirisha abiria hadi saa tatu au saa nne usiku ambapo hufunga mahesabu na kwenda kupumzika majumbani mwao.

Hali ni mbaya zaidi kwa madereva  wa mabasi makubwa yanayofanya safari zinazoenda masafa marefu ambao hulazimika kusafiri kwa muda mrefu jambo linalowasababishia maumivu ya mgongo kwa muda mrefu.

Mohamed Juma dereva wa magari ya masafa marefu anasema yeye amezoea kusafiri umbali mrefu huku akitumia mbinu mbalimbali ikiwemo kulala chali kwa muda wa nusu saa akifika nyumbani.

“Sisi madereva wa magari ya masafa marefu ndio tunapata sana shida ya mgongo kwa sababu tunakaa barabarani masaa mengi ndio maana nikifika tu nyumbani naoga kisha natafuta sakafu safi najilaza chali hata kwa nusu saa,” amesema Juma.

Licha ya maumivu hayo, madereva hao wanakiri kutokwenda hospitali wala kumeza dawa, baadhi yao hutumia mbinu za asili kama kulala sakafuni kwa muda mrefu.

“Kwenda hospitali sijawahi, maumivu yakizidi au nikirudi tu kutoka kazini huwa nalala chali sakafuni kwa muda wa nusu saa au zaidi kisha mgongo unakaa sawa na kesho yake naweza kuingia kazini bila shida,” amesema  Mohamed.

Kwa upande wake Kirway anasema maumivu yakizidi huzungumza na mke wake ambaye humfanyia ‘massage’ au kama hayupo hufanya mazoezi mepesi ikiwemo ya kujinyoosha.

Wingi wa abiria huwafanya madereva kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika hivyo kuongeza uwezekano wa kupata maumivu ya mgongo.Picha|World My Feet.

Mtindo wa maisha ndiyo sababu

Dk Joshua Sultan, mtaalamu wa afya wa kujitegemea ameiambia Nukta Habari kuwa mtindo mbovu wa maisha huchochea zaidi maumivu ya mgongo kwa madereva wengi kutokana na baadhi yao kutojenga utamaduni wa kufanya mazoezi mepesi na yale ya kunyoosha mgongo baaada ya kuendesha gari kwa muda mrefu.

“Unakuta dereva anakaa chini kwa saa nane au zaidi hajipi muda wa kujinyoosha katikati ya hayo masaa na bado utakuta anakunywa pombe na hafanyi mazoezi,” amesema Dk Sultan.

Kwa mujibu wa daktari huyo kila baada ya masaa 3 au manne madereva wanatakiwa kujipa muda wa kupumzika kwa kushuka kwenye magari kujinyoosha na kutembea ili kubadili mkao wa pingili za mgongo ambazo zikiathirika husababisha maumivu hayo.

Amebainisha kuwa licha ya madereva hao kuchukulia tatizo hilo kama sehemu ya maisha yao, wanatakiwa kumuona daktari pale maumivu hayo yanapodumu kwa saa 48 mfululizo au zaidi.

“Ukishaona una maumivu makali kiasi cha kushindwa kukaa, kulala au kufanya shughuli yoyote kwa siku tatu mfululizo  na hayasikii dawa unatakiwa kumuona daktari mara moja ili kupata matibabu,” ameongeza Dk Sultan.

Dk Sultan ameyataja madhara ya kukaa na maumivu hayo kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kusababisha ulemavu na kupata matatizo ya kudumu ya pingili za mgongo.

Suluhu hii hapa

Ili kuondokana na matatizo hayo Dk Sultan ameshauri madereva kubadili mtindo wa maisha kwa kuingiza mazoezi katika ratiba zao za kila siku  na kupunguza unywaji wa pombe.

“Naasisitiza sana hawa madereva waache pombe na ule muda wanaotumia kunywa baada ya kazi wawekeze katika kufanya mazoezi na kuiweka miili yao sawa,” amesema Dk Sultan.

Aidha, amewashauri pia kuacha ulaji usiofaa ambao kwa mujibu wake husabaisha uzito mkubwa ambao  wakati mwingine huchangia maumivu ya mgongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks