Kabudi: Waliong’oa viti Benjamini Mkapa walipe
- Viti 156 vya bluu na 100 vya rangi ya chungwa vyang’olewa.
- Ni kutokana na fujo zilizoibuka kati ya mashabiki wa Simba na wa Club Sportif Sfaxien ya Tunisia.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kuwaandikia barua klabu ya Simba ya kulipa gharama za uharibifu wa viti katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo Desemba 16, 2024 nakala ya barua hiyo iende kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Agizo la Kabudi limefuatia mara baada ya kuibuka kwa vurugu baada ya kumalizika kwa mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika iliyochezwa jana Desemba 16, 2024 katika Uwanja wa Mkapa kati ya Simba Sport Club dhidi ya Club Sportif Sfaxien ya Tunisia.
Vurugu hizo zilitokea mara baada ya mashabiki wa Club Sportif Sfaxien kutoridhishwa na maamuzi ya refa wa mchezo huo kuchezesha zaidi ya dakika saba za nyongeza jambo lililosababisha Simba kupata goli la ushindi ambapo kwa mujibu wa picha jongefu baadhi ya wachezaji na benchi la ufundi la Sportif Sfaxien walimfuata refa na kuanza kumshambulia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Muliro J. Muliro katika fujo hizo shabiki mmoja wa timu ya Sportif Sfaxien aliumia na kupatiwa huduma ya kwanza huku viti vya rangi ya bluu 156 na chungwa 100 viking’olewa.
Aidha, Waziri Kabudi amewataka mashabiki wanaoingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.
“Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubaliki na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja na kuwaandikia Simba Sports Club na TFF, wapeni ushirikiano Polisi ili watu wote waliokuwa wanang’oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria, lazima tabia hii ikomeshwe” amesema Prof. Kabudi.