Wanawake wanavyojidhuru sehemu nyeti kuwasahau wapenzi wao
- Ni muhimu kujipenda na kutokuwa na matarajio makubwa katika mahusiano.
Dar es Salaam. “Toka nakuwa sikuwahi kuhisi maumivu ambayo niliwahi kuyapata siku nimeachwa. Nilihisi moyo unatoka, nilipiga simu zaidi ya mara 100 anakata yaani acha tu,”
Haya ni maneno ya Awalina Saidy, mfanyabiashara wa vipodozi Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambaye aliachwa na mpenzi wake miaka miwili iliyopita.
“Nilikuwa kama mjinga siku hiyo, kila nilichokuwa nafanya kilisimama nilioona dunia ni ndogo,nililia sana kiasi kwamba macho yalivimba kwa siku tatu ila baadae nikaona mambo yasiwe mengi nikakubali matokeo,” anasema Awalina.
Awalina ni miongoni mwa wanawake wengi ambao huachwa na wapenzi wao wakiwa katika mahusiano rasmi (ndoa) na yasiyo rasmi kwa sababu mbalimbali.
Baada ya kuachwa, hufanya maamuzi tofauti ili kuziponya hisia zao na kurejea katika hali ya kawaida na kuendeleza maisha yao ikiwemo kulipiza kisasi, kujiua au kupotezea.
Mkazi wa Tanga, Maria Amosi anasema wakati mume wake anamuacha alitamani kujiua ili asahau kila kitu.
“Aliniacha kwakua sizai ila najiuliza kwani mtoto natoa mimi si Mungu na vipi kama mimi sikuwa na shida wewe acha tu siku hiyo nililia sana ila kwa sasa nimeshazoea hata nikisikia taarifa zake naona kawaida tu,’’ anasema Maria ambaye aliachika kwa sababu hakuzaa watoto.
Baada ya maumivu ni kawaida kwa watu kuhisi hawana sababu ya kuendelea kuishi,jambo linaloweza kupelekea mhanga kujaribu kufanya lolote ili kuwa sawa. Picha / Shutter stock.
Ni zaidi kupotezea na kujiua
Baadhi yao huamua kujidhuru sehemu za miili yao kama hatua ya kuwasahau wapenzi wao pasipo kufahamu madhara ya kiafya wanayoweza kuyapata.
Daktari wa magonjwa ya binadamu kutoka mkoani Morogoro, Dk Philipo Isaku ameiambia nukta.co.tz kuwa katika majukumu yake ya kitabibu amekuwa akistajaabishwa na wanawake wanavyojidhuru miili yao ILI kusahau mahusiano yaliyopita.
Dk Isaku ambaye amewahi kukaa nchini Comoro kwa takribani miaka 12 kabla hajarejea Tanzania anathibitisha kuwatibu mabinti watano na wote wakiwa na majeraha katika sehemu nyeti za miili yao.
“Kuna wadada waliletwa kwangu kutibiwa nikiwa hospitali, ila kitu kilichonishangaza zaidi ni kuwa majeraha yao yote yapo katika sehemu ambazo ni nadra sana kuyapata majeraha hayo na ukiwa kama daktari lazima umuulize mgonjwa shida nini…”
“…Hivyo nilivyowauliza wakaniambia kuwa wamesalitiwa kwenye mahusiano na wanaume waliokuwa nao ndio maana wakachukua hatua hizo ili kuwasahau,” anasema Dk Isaku.
Mtaalam huyo wa afya ya binadamu anaeleza kuwa mabinti wa nchi hiyo hutumia njia mbalimbali kujidhuru katika miili yao kama ishara ya kuwasahau wapenzi wao wakati nchini Tanzania wao huona njia sahihi ni kuchukua maamuzi ya kukatisha uhai wao kwa kujinyonga, kumeza sumu au kumeza vidonge vingi.
“Mmoja wa mabinti hao alichukua mafuta ya taa na kujimwagia sehemu za siri na kisha akaichoma moto kitendo hicho kilifanywa na mabinti wengine wanne na wa tano yeye aliamua kuchoma maziwa yake ili tu iwe alama ya kumsahau mtu aliyemuumiza,” anasema Dk Isaku.
Madhara ya kiafya ambayo aliyejidhuru anaweza kupata ni pamoja kifo, ulemavu na majeraha ya muda mrefu ambayo yanaweza kumkosesha fursa ya kuingia katika mahusiano mengine.
Mapenzi yanaweza kuwa mazuri, ila yanapogeuka kuwa shubiri watu wengine hufikiria kifo kuwa ndio suluhu la mwisho. Picha / istock.
Dk Isaku ameongeza kuwa kuna sababu nyingi ambazo husababisha mahusiano hayo kuvunjika ikiwemo, kukosa uaminifu kati ya wenza, marafiki kuingilia mahusiano, mazingira ya familia na shinikizo la jamii.
Pia matarajio makubwa kabla ya kuingia kwenye mahusiano pamoja na kutojali na kutoheshimiana.
Mtaalam wa saikolojia na mahusiano kutoka jijini Dar es Salaam, Patrick Motto anasema kuwa watu wengi wamekuwa wakiingia kwenye mahusiano ambayo hawajua historia za wenza wao kitu ambacho huchochea wanawake kuachwa na kuumizwa.
Wanaume wanajidhuru?
Mahusiano yaliovunjika huku mwanamke akimuacha mwanaume akiwa mwenye huzuni. Picha / Newsweek.
Dk Isaku ambaye ana utaalam wa mahusiano anaeleza kuwa mara nyingi wanaume huchukua maamuzi ya kutaka kumdhuru mwanamke kwa lengo la kumuua, kujiua mwenyewe au kumuua mwanamke na kujiua na yeye mwenyewe.
“Kuna wakati unaona bora tu nipambane na familia yangu inayonisaidia wakati wa shida kuliko kuwa na wanawake, kuna muda unakuta sina pesa na mtu anataka pesa ukimnyima au ukisema sina nivumilie anakwambia humpendi jamani aaah!, acheni tu si bora ukae pekee yako Mungu atamleta atakaye nifaa,’’ anasema Abubakari Kimbendo, mkazi wa Morogoro.
Suluhu yake hii hapa?
Tovuti ya Psychology Today inaeleza kuwa ili kuhakikisha mahusiano yanakuwa imara na kupunguza madhara ya kuachana hasa kwa wanawake, wapenzi wajenge utamaduni wa kuwasiliana na kushughulikia changamoto zao.
Pia wote wawili lazima wawe na dhamira ya kukubaliana na tofauti zao, hata kama zitabadilika kwa muda.
Mtaalam wa saikolojia na mahusiano kutoka jijini Dar es Salaam, Patrick Motto anasema kuwa kitu cha kwanza ambacho mwanamke anatakiwa kufanya anapokuwa ameachwa ni kujipenda yeye zaidi kuliko kumpenda mtu mwingine yoyote.
“Kuwa ‘selfish’ (mbinafsi) kwa ajili ya maisha yako sio mbaya kiasi kwamba hata mtu anapokuja kwenye maisha yako hakuti ‘emotional gap’ (pengo la kihisia), hata mtu akikuaacha maumivu hayatakaa muda mrefu kivile kwa sababu unajipenda wewe mwenyewe,” anasema Motto.
Ni vyema kujipa mapumziko unapohisi akili haiwezi kufikiri tena baada ya kupitia maumivu ya mapenzi. Picha / Bestcollege.com.
Pata muda wa kupumzika
Jipe mapumziko la kupona majeraha ya mahusiano yako ya zamani kabla ya kuanza mahusiano mapya na usichukue maamuzi yoyote ya kujidhuru kimwili wala kihisia.
“Wewe mtu unaachwa leo wiki ijayo unaingia kwenye mahusiano hata wewe mwenyewe haujipi ‘break’ (mapumziko) unajikuta kwamba kila siku stori ni ile ile kwa sababu kama umeachwa labda kwa ajili ya tukio fulani lakini huwezi kuuliza kwanini huyu mtu kaniacha utajirekebisha unajikuta kila siku upo kwenye mstari ule ule,” anasisitiza Motto.
Hakikisha unajua kuwa wewe ni wa thamani kuliko hata mahusiano yanayokuumiza na usiwe na matarajio makubwa kwenye mahusiano.
“Hii itakusaidia kuelewa aina ya mtu uliyenaye je ni mtu wa kupokea tu au anarudisha anachokipata kutoka kwako na ni kwa sababu watu wengi wanaingia kwenye mahusiano wakiwa na matarajio makubwa huku wakisahau kuwa mtu anayekuwa naye kalelewa katika mazingiara tofauti,” anasema Motto.
Hisia hazidanganyi moyo unapoumia, machozi huongea. Picha / The Indiependent.
Mtaalam wa Saikolojia na Mahusiano kutoka mkoani Tanga, Leyla Abubakari anasema kuwa ni muhimu mtu kukubali changamoto za kimaisha na kuzingatia kuwa kuachana na watu ni sehemu ya safari ya maisha.
“Kuna nyakati ambapo utaachana na watu muhimu, na hii haimaanishi kwamba hawakuthamini. Unapaswa kutambua kwamba huenda kwa wakati huo watu hao hawakuhitaji katika maisha yao, na hiyo ni kawaida,” anasema Leyla.
Kutokujilaumu kwa sababu ya kuachwa
“Kumbuka, kama mtu huyo alikusudiwa kuwa sehemu ya maisha yako, basi Mungu asingekuruhusu muachane, wakati mwingine, kuachana ni njia ya maisha inayo kupeleka katika mwelekeo bora zaidi, Hata kama ulifanya makosa katika mahusiano, kujilaumu kupita kiasi hakutakusaidia badala yake, ni nafasi ya kujifunza kulingana na makosa,” anasema Leyla.
Mapenzi yasikufanye ukahisi kuwa hakuna mtu yoyote upande wako na kujivisha lawama zote mwenyewe. Picha / Pngtree.
Kukubali hisia za maumivu
Leyla amebainisha kuwa ni muhimu kukubali kwamba unahisi maumivu, kubali huzuni, hasira, au hata kuchanganyikiwa kiasi, lakini usikubali hisia hizo zikukamatie milele. Ipe muda nafsi yako kupitia maumivu hayo ni sehemu muhimu ya uponyaji.
Kubaki umekwama katika nguvu za majeraha kunazuia mabadiliko na kupuuza zawadi kubwa zilizomo ndani ya majeraha. Picha / Circles.
Jishughulishe na kufanya mazoezi
Hii husaidia kupunguza msongo wa mawazo kwa kutoa homoni aina ya ‘endorphins’, ambazo ni vichocheo vya asili vya furaha.
Pia, kujishughulisha na shughuli kama kujifunza kitu kipya, kusoma vitabu, au kutembelea marafiki kunaweza kusaidia kujiepusha na mawazo hasi.
Kupona baada ya maumivu ni hatua ambayo kila mtu aliyeumizwa anapaswa kujiandaa nayo ikiwa ni pamoja na kufanya vitu vinavyomfanya kuwa na muelekeo mpya wa maisha. Picha / V3 Apparel.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wanasaikolojia hao wanasisitiza kuwa kabla ya kuingia katika mahusiano ni vyema kuzingatia historia zao za utotoni ambazo ndio njia kuu ya kuanza kujua udhaifu wa mtu.