Dk Mpango atoa maagizo kudhibiti maambukizi ya Ukimwi kwa vijana Tanzania
- Ataka vijana kujitambua lakini pia kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
- Aitaka TACAIDS, wizara za kisekta kudhibiti mazingira ya kuenea kwa VVU.
Dar es Salaam: Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Phillip Mpango ametaka hatua zichuliwe kunusuru vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24 wakiwemo wasichana ambao wamebainika kuongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) Tanzania.
Dk Mpango ametoa maagizo hayo Desemba 1, 2024 katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Phillip Mpango akirejea ripoti ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya VVU na UKIMWI (Tanzania AIDS Impact Survey – THIS) 2023/24 amesema kuwa kundi la vijana hasa wa kike ndilo kundi ambalo lipo hatarini zaidi ya kupata VVU.
Mpango ameitaka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), wizara za kisekta pamoja na wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla kuweka mkazo katika kudhibiti mazingira yanayochochea maambukizi ya VVU hasa kwa vijana,
Pia amewataka vijana kujitambua na kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na kuwataka vijana ambao tayari wanaishi na maambukizi waendelee kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo (ARV) ili kuimarisha afya zao.
“Natoa wito kwa vijana kujitambua lakini pia kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.” amesema Dk Mpango.
Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani. Picha |Ruvuma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika maadhimisho hayo ameeleza kuwa Serikali imeweka msisitizo kwa vijana kuendesha mijadala na kuanzisha vilabu vya masuala ya Ukimwi mashuleni ili kuwezesha vijana kujua na kupata elimu ya ugonjwa huo.
“Ni jukumu la vijana sasa kuzingatia na kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi” amesema Majaliwa.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama akizungumzia ripoti hiyo amesema kiwango cha ushamiri wa VVU kimepungua kitaifa kutoka asilimia 7 mwaka 2003/04 mpaka asilimia 4.4 mwaka 2022/23.
Amesema kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 8.1 mwaka 2023.
Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa Disemba 1 kila mwaka huku lengo la maadhimisho hayo likiwa ni kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki katika ajenda ya udhibiti Ukimwi, kutathmini muelekeo wa kudhibiti VVU na kutafakari changamoto, mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya udhibiti wa VVU.