Kesi ya dereva wa basi lililoua tisa Mwanza yapigwa kalenda
- Hakimu ataja sababu ya kuahirisha kesi hiyo kuwa ni afya ya mstakiwa kutokuwa sawa.
Mwanza. Kesi inayomkabili aliyekuwa dereva wa basi la Asante Rabi Shedrack Swai (37) aliyesababisha ajali iliyoua watu tisa katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, imehairishwa hadi Novemba 11 mwaka huu baada ya mshtakiwa kudai afya yake haiko sawa.
Mtuhumiwa huyo anayeshtakiwa kwa makosa 64 ikiwemo kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya umma Mwanza- Shinyanga na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali amepandishwa kizimbani leo Novemba 5, 2024 kwa mara ya pili mbele ya Ester Maliki Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi.
Baada ya kupandishwa kizimbani Swai aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo na kupangiwa tarehe nyingine kwa kunyanyua mkono na kuruhusiwa kuzungumza kabla ya kuanza kusomewa hoja za awali na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Lilian Meli ambapo baadae hakimu Ester Maliki aliridhia ombi hilo.
“Kwa kuwa mshtakiwa ameomba kuwa hali yake kiafya siyo nzuri basi tunaahirisha shauri hili hadi tarehe 11 Novemba 2024,” amesema Hakimu Ester.
Dereva wa basi la Asante rabi Shedrack Swayi (37) akiingia mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka kwa mara ya pili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Misungwi. Picha| Mariam John/Nukta.
Kwa sasa mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya wadhamini wake kutimiza masharti ya dhamana.